Monday 7 October 2013

BoT yazungumzia kasi ya uporaji mabenki


Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam,
 Kamishna Suleiman Kova

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imezungumzia kasi ya kuvamiwa na kuporwa fedha kwenye mabenki nchini na kutoa ushauri wa jinsi ya kukabiliana na matukio hayo.

BoT imewashauri wadau, vikiwamo vyombo vya ulinzi na usalama, kutumia fursa iliyopo kujadiliana, ili kuupatia ufumbuzi udhaifu unaotoa mwanya kwa matukio ya ujambazi ya kuvamia na kupora fedha kwenye mabenki, kuendelea kushika kasi nchini.

Meneja Usimamizi wa Mabenki wa BoT, Agapiti Kobelo, alitoa ushauri huo, alipozungumza katika mahojiano maalum na NIPASHE.


Alisema suala la kuimarisha ulinzi ni nyeti kwa anayefanya shughuli za benki, kwa kuwa matukio ya ujambazi, ni changamoto kubwa inayozikabili taasisi za fedha si Tanzania tu, bali katika nchi zote duniani.

“Hivyo basi, mabenki, BoT ikiwa ni mdhibiti (wa taasisi za fedha) na vyombo vya ulinzi na usalama wanapaswa kujifunza matukio (ya ujambazi) yanayotokea, udhaifu uliko na kuweka mikakati ya kuimarisha ulinzi kwenye mabenki,” alisema Kobelo.


Hata hivyo, alisema suala la ulinzi ni jukumu la benki kwa sababu ndiyo inayotunza fedha, ambazo zinatakiwa na watu wote; wakiwamo raia wema na waovu.
Hivyo, akasema tatizo la ujambazi ni changamoto, ambayo yeyote anayefanya shughuli za benki anaweza kukumbana nayo.

Kutokana na hali hiyo, alisema kuna haja kwa wadau kufanya uchunguzi kubaini uliko udhaifu unaoruhusu changamoto hiyo na kuipatia ufumbuzi.

Alisema pamoja na mambo mengine, uchunguzi huo unapaswa kuja na majibu sahihi iwapo uwezo wa polisi utatosheleza mahitaji ya ulinzi kwenye mabenki na kama kuna udhaifu wowote kwenye kampuni binafsi za ulinzi zinazofanya kazi hiyo katika maeneo hayo. 

BoT ambayo pamoja na majukumu yake mengine ni msimamizi wa mabenki yote nchini, imetoa kauli hiyo  wakati huu ambao  matukio ya benki kuvamiwa na majambazi na kuporwa mamilioni ya fedha yameshamiri.

Matukio hayo yamezua mjadala mkubwa katika jamii na kuwafanya wananchi kuhoji umakini wa vyombo vya ulinzi vilivyopewa jukumu la kulinda benki hizo.

Katika hali inayozua maswali ambayo hadi sasa Watanzania hawajapata majibu, ni kwamba majambazi  wanaozivamia benki hizo wamekuwa wakitumia silaha za moto yakiwamo mabomu pamoja na kuvalia sare za polisi kufanikisha ujambazi huo.

Katika kipindi cha kuanzia Agosti hadi Septemba mwaka huu, matukio makubwa matatu ya benki kuporwa yalitokea katika jiji la Dar es Salaam ambalo limeshamiri kwa matukio hayo.

Tukio la kwanza lilitokea Agosti 29, mwaka huu baada ya watu wanne wanaosadikiwa kuwa majambazi wakiwa na silaha za moto mmoja akiwa amevalia sare za jeshi la polisi na simu ya upepo kuvamia benki ya Habib iliyopo Kariakoo na kupora Sh. 1,076,653,700.

Septemba 6, mwaka huu, majambazi walivamia benki ya Commercial Bank of Africa (CBA) tawi la barabara ya Nyerere na kuiba zaidi ya Sh. milioni 350 pamoja na fedha za kigeni Dola za Marekani na Euro.

Tukio la Tatu lilitokea Septemba 28 mwaka huu baada ya majambazi waliovalia sare za Jeshi la Polisi walipovamia benki ya I& M jijini Dar es Salaam na kuiba zaidi ya Sh. milioni 150.

Tukio jingine lililotokea Julai 30, mwaka 2009, baada ya benki ya NMB tawi la Temeke kuvamiwa na majambazi waliokuwa na mabomu na kuiba zaidi ya Sh. milioni 150 na kujeruhi watu 13 waliokuwamo ndani ya benki hiyo wakiwamo askari wawili.

Majambazi hayo baada ya kufanikisha uporaji huo halikimbia kwa kutumia magari yaliyokuwa na namba za SU na STJ.

Kufuatia kukithiri kwa matukio ya uhalifu  wa  kupora fedha kwenye mabenki, Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova, alitangaza kwamba ulinzi katika benki zote  sasa utafanywa na polisi.

Alisema uamuzi wa kulinda benki umefikiwa kufuatia mkutano kati yake na makamanda wa Polisi wa mikoa wa kanda hiyo.

Kamannda Kova alisema wamekubaliana mambo kadhaa ili kuhakikisha uhalifu huo unaofanywa na magenge ya kihalifu unadhibitiwa na kwamba makamanda hao wametakiwa kuhakikisha kuwa wanashiriki kikamilifu katika utekelezaji wake.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...