Friday 4 October 2013

Mbagala yachemka

Baadhi ya wakazi wa Mbagala jijini Dar es Salaam, wakiwa wamefunga barabara kwa mawe baada ya mwanafunzi wa shule ya msingi eneo hilo kugongwa na gari na kufariki dunia jana

Wakazi wa Mbagala jijini Dar es Salaam jana waliasi kwa takribani saa nne na kuilazimisha dola kuingilia kati kwa kutumia mabomu kukabiliana nao.

Polisi walifyatua mabomu ya machozi kuwakabili wananchi hao ambao walikuwa wakifanya ghasia na kufunga barabara ya Kilwa kwa saa nne.

Tukio hilo lilitokea kuanzia saa 4:30 asubahi katika eneo la Mbagala Kizuani baada ya wananchi hao kulala barabarani kuishinikiza serikali iweke matuta kwenye eneo hilo katika barabara ya Kilwa.

Wananchi hao waliokuwa na hasira walichukua hatua hiyo kufuatia tukio la  mtoto mmoja mwenye mri wa miaka 10 ambaye jina lake halijafahamika, kugongwa na lori wakati akijaribu kuvuka barabara na kufa papo hapo.


Kutokana na tukio hilo, magari yaliyokuwa yanakwenda na kurudi mikoa ya kusini pamoja na daladala yalisitisha safari zao kwa muda na kusababisha msongamano mkubwa kwa saa kadhaa.

Baadhi ya watu waliokuwepo eneo la tukio, waliliambia NIPASHE kwamba mtoto huyo anayesemekana ni mwanafunzi wa Shule ya Msingi Mbagala Kizuiani, aligongwa wakati akivuka barabara kwenda shuleni kwake.

Walisema  matukio ya watu kugongwa na kufa yamekuwa yakitokea kila mara na hakuna juhudi zozote zinazofanyika za kuzuia ajali hizo.

Baada ya kutokea ajali hiyo, wananchi walionekana kupandwa na hasira walionekana wakiwa wamelala barabarani na kuweka vizuizi vya matofali ili kuishinikiza serikali ijenge matuta eneo hilo.

Rajabu Msumi, mkazi wa eneo hilo, aliliambia gazeti hili kuwa kilichowafanya kuchukua hatua hiyo ni kuchoka baada ya kuona maisha ya watu yakikatishwa kila siku na madereva wazembe.

“Kila siku watu wanakufa, lakini hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa leo (jana) imefika mwisho, tutalala hapa hadi tuwekewe tuta,” alisema Msumi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Engelbert Kiondo, alipofika eneo la tukio alijaribu kuwatuliza wananchi kwa kuwaomba watoke barabarani ili ombi lao la kuwekewa matuta litatuliwe.

Kamanda Kiondo aliwaambia wananchi kwamba serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) imekubali kuweka matuta kama wanavyotaka, lakini kwanza wafungue barabara ili kuwawezesha wataalamu wafike eneo hilo.

“Hatuwezi kufunga barabara huku tukitaka tuwekewe matuta, lami haiwezi kuja kwa ndege au bodaboda, jambo la msingi tuifungue ili wahusika waje hapa na kufanya tathmini,” Kamanda Kiondo aliwaambia wananchi hao.

Hata hivyo, kauli ya Kamanda huyo haikuwaridhisha wananchi hao, ndipo kundi moja la lilijitokeza na kuanza kuchoma matairi juu ya barabara hiyo.

Kutokana na kitendo hicho, polisi waliamua kuingilia kati kwa kulipua mabomu ya machozi na kusababisha watu kukimbia ovyo kunusuru maisha yao.

Aidha, katika tukio hilomtu mmoja alikamatwa na kupelekwa katika kituo cha Polisi cha Maturubai akituhumiwa kuhusika na uchomaji moto kwenye barabara hiyo.

UTATA WA MWANAFUNZI
Juhudi za kupata jina la mtoto aliyekufa katika ajali hiyo hazikuzaa matunda baada ya mwalimu mmoja aliyeonekana kwenye ofisi ya mwalimu mkuu wa shule hiyo ambaye hakutaja jina lake, kusema kuwa  hakuna mwanafunzi wake aliyefariki.

“Sina mwanafunzi aliyekufa kwa gari leo,” alisema kwa mkato.

Kamanda Kiondo alipoulizwa kuhusu mtoto huyo, alisema bado wanaendelea na uchunguzi wa suala hilo na atalitolea taarifa baadaye.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...