Wednesday, 27 November 2013

MANYARA KINARA UKEKETAJI WANAWAKE KASKAZINI

Mgeni Rasmi katika Uzinduzi huo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu Kanda ya Moshi,Aisha Nyerere

Mkoa wa Manyara unaongoza kwa Kanda ya Kaskazini kwa ukeketeaji wanawake.

Takwimu hizo zilitolewa juzi na  Mkurugenzi wa Mtandao wa kuelimisha Jamii juu ya madhara ya Ukeketaji (NAFGEM), Francis Selesini wakati wa   uzinduzi wa Maadhimisho  ya Kimataifa ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia zinazofanyika kwa Kanda hiyo mkoani Kilimanjaro.

 Selesini alisema kuwa takwimu zinaonyesha kuwa kati ya wanawake 100 mkoani humo, 71 wamefanyiwa ukeketaji.

Selasini alisema takwimu hizo zimetolewa baada ya utafiti huo uliofanywa na serikali kwa kushirikiana na shirika la kimataifa linaloshughulika na  watoto (Unicef) kuhusu athari za ukeketaji.

“Hili ni tatizo kubwa sana,” alisema Selasini.

Alisema pia utafiti umebaini kuwa kati ya wanawake 60 kati ya 100 wamefanyiwa vitendo hivyo vya kikatili mkoani  Dodoma.
  Aliitaja sababu ya kukithiri kwa vitendo hivyo kuwa ni mila na desturi za makabila yanayoishi katika mikoa hiyo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya maadhimisho hayo kwa kanda hiyo,  Elizabeth Mushi, alisema chimbuko lake ni mauaji ya ikatili ya wadada 14 wa Mirabelle  yaliyotokea mwaka 1960 nchini Dominika.

“Lengo kuu la kufanya maadhimisho haya ni kujenga uelewa kuhusu unyanyasaji wa kijinsia kama uvunjaji wa haki za binadamu kijamii, kikanda, kitaifa na kimataifa, tunatumia siku hizi kuimarisha kazi za kupinga unyanyasaji dhidi ya wanawake katika ngazi za chini na kujenga daraja kati yao na haki zao, ” alisema.

Mgeni Rasmi katika Uzinduzi huo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Aisha Nyerere, alisema  ukatili ni kitendo cha aibu na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.

Jaji Nyerere alisema  serikali imepitisha sheria ya kujamiana na adhabu yake inafikia hata kifungo cha maisha jela. 

Kauli mbiu ya Maadhimisho hayo kwa mwaka huu ambayo kitaifa yanafanyika jijini Dar es Salaam ni   Funguka, tumia mamalaka yako, zuia ukatili wa kijinsia kuboresha afya ya jamii. 
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...