Thursday, 14 November 2013

MAPYA YAIBUKA MAUAJI YA MVUNGI


Rais Jakaya Kikwete, akimfariji mjane wa marehemu Dk. Sengondo Mvungi, Anna, baada ya kwenda nyumbani kwake Mpiji Magohe, Wilaya ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam jana.(PICHA:OMAR FUNGO

Mwanafamilia afunguka anachokijua
Familia ya aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Sheria, Dk. Senkondo Mvungi (61), imesema watu waliosababisha kifo chake walipoingia ndani cha kwanza walitaka kompyuta mpakato (laptop) na nyaraka muhimu.

Mmoja wa wanafamilia hiyo (jina limehifadhiwa) akizungumza na NIPASHE nyumbani kwa marehemu Dk. Mvungi, eneo la Mpiji Magohe, alisema hadi sasa wako kwenye kiza kinene juu ya lengo la waliosababisha kifo cha ndugu yao.

Akielezea mazingira ya siku ya tukio, alisema watu hao walivunja mlango wa nyuma ambao unaingia jikoni na kumkutana kijana msaidizi wa Dk. Mvungi na kumkamata na kwenda naye hadi sebuleni.

“Walimkamata na kupanda naye hadi sebuleni, Dk. Mvungi alisikia purukushani na kuamua kutoka akiwa hana silaha yoyote, walipomwona walimfuata na kumng’angania huku wakisema wanataka laptop yake na nyakara muhimu,” alisema.



Alisema watu hao walikuwa wanne na hawakuficha sura zao na kwamba Dk. Mvungi hakukubaliana nao haraka na katika zogo hilo, mmoja wa watu hao alijeruhiwa kichwani na kuanza kuchuruzika damu.

“Baada ya mwenzao kutokwa na damu mmoja alisema hapa si salama akatoa panga na kumkata mara tatu Dk. Mvungi ambaye alianguka chini na walikwenda kwenye kabati na kutoa komyuta na nyaraka mbalimbali, bastola ya marehemu na kisha kumfuata mke wa marehemu wakitaka fedha wakachukua fedha kwenye kabati na kuondoka,” alisema.

Aidha, ndugu huyo alisema anashangazwa na taarifa za polisi kuonyesha mapanga na kigoda pekee, huku kompyuta haijulikani ilipo na watu hao tangu wanaingia walihitaji kompyuta na nyaraka muhimu.

“Ni vyema Polisi wakafanya uchunguzi wa kina kwani inaonekana lengo la watu hawa halikuwa fedha, walizichukua mwishoni kabisa baada ya kupata kompyuta na nyaraka hizo na kisha kutokomea,” alisema mwanafamilia huyo.

Alisema eneo hilo halina umeme wa Tanesco bali wanatumia umeme wa jua na kwa siku hiyo taa ya nyuma ilikuwa haiwaki.

MAJIRANI WANASEMAJE?
Baadhi ya majirani walisema kuwa kwenye eneo hilo imekuwa kawaida watu kuvamiwa na kujeruhiwa kutokana na ukweli kuwa hakuna kituo cha polisi na umeme.

“Umeme umeishia eneo la mbali sana na hatuna kituo cha polisi hadi eneo la Mbezi kwa Yusuph, hivi karibuni kuna familia mbili zilivamiwa na kuporwa fedha na kupigwa kwa ubapa wa panga…tunaiomba serikali kutufikiria tunahitaji kituo cha polisi,” alisema Hamida Ally, mkazi wa eneo hilo.

Aidha, alisema baadhi ya mafundi si waaminifu wanavujisha siri za familia wanazofanyia kazi za ujenzi hasa siku wanazolipwa fedha na kwamba kwa kuwa Dk. Mvungi alikuwa anaendelea na ujenzi wa uzio wa nyumba yake walijua ana kiwango kikubwa cha fedha.

SIMANZI NYUMBANI KWAKE

Hali ya simanzi imetanda nyumbani kwake huku viongozi wa serikali, vyama vya siasa, majirani na jamaa wakijumuika na familia ya Dk. Mvungi kuomboleza na kuwafariji.

Nyumba yake ina uzio unaoendelea kujengwa ambao haujafika nusu huku eneo kubwa likiwa wazi.

WARIOBA AWASALI

Mwenyekiti wa Tume ya mabadiliko ya Katiba mpya, Jaji Joseph Warioba, aliwasilia majira ya saa 6:45 akiwa ameambatana na wajumbe wa Tume hiyo ambao walikwenda kutoa pole kwa wafiwa na mjane wa marehemu na kuweka saini kwenye kitabu cha maombolezo.

Viongozi wengine ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadik na Mkuu wa wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana.

Wengine ni Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe na Naibu Waziri wake, Angela Kairuki.

Mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi na Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia, ndiye aliyesimama kwa niaba ya familia, chama na taasisi alizowahi kuzifanyia kazi Dk. Mvungi kuzungumzia taratibu za mazishi.

KIKWETE NA SALMA
Aidha, Rais Jakaya Kikwete na mkewe Mama Salma, waliwasili majira ya saa 7:35 mchana, ambaye alikwenda moja kwa moja kutoa pole kwa wafiwa na kusaini kitabu cha maombolezo.

Rais Kikwete alitoa pole kwa wajumbe wa Tume na majirani waliokuwapo na kuondoka.

Kwa mujibu wa Mbatia, Dk. Mvungi ameacha mjane Anna Mvungi na watoto Dk. Natujwa Mvungi, Injinia Doreen Mvungi, Nakundwa Mvungi na Adrian Mvungi.

RATIBA YA MAZISHI
Kwa mujibu wa ratiba ya mazishi ya kiongozi huyo, mwili wake unatarajiwa kuwasili nchini kesho.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, taratibu za kuusafirisha mwili wa Mjumbe wake, zimekamilika.

Ilisema baada ya kuwasili, mwili huo utahifadhiwa katika Hospitali ya Jeshi Lugalo iliyopo jijini Dar es Salaam.

Keshokutwa mwili utapelekwa katika Kanisa  Katoliki la Mtakatifu Joseph kwa ajili ya ibada saa nne asubuhi, kisha utapelekwa viwanja vya Karimjee kwa ajili ya kutoa heshima za mwisho hadi saa 11 jioni na baadaye utapelekwa nyumbani kwake Msakuzi, Mpigi Mahohe.

Jumapili utasafirishwa kwenda kijijini kwao Kisangara Juu, wilayani Mwanga ambako ndiko utazikwa Jumatatu ya Novemba 18, mwaka huu.

Dk. Mvungi alizaliwa Novemba Mosi, mwaka 1952 na alijeruihiwa siku mbili baada ya kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa.

Dk. Mvungi alikulia katika maisha ya kawaida, katikati ya jamii ya wakulima, huko Kisangara Juu, Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro.

Ni mtoto wa pili kutoka kitindamimba katika familia ya watoto saba ya baba yao aliyekuwa mkulima wa kahawa, mahindi, ndizi, mihogo na maharage na pia mzee huyo alikuwa mfugaji wa ng’ombe wa maziwa.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...