Dar es Salaam. Siku 23 baada ya Nelson Mandela kuachiwa huru kutoka gerezani, Februari 11, 1990 aliwasili hapa nchini kwa ziara fupi iliyokuwa na msisimko wa aina yake.
Aliwasili nchini Machi 5, 1990 na kulakiwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Dar es Salaam (Sasa Uwanja wa Julius Nyerere) na Mwalimu Nyerere.
Baada ya kuwasili, alikagua gwaride kama ilivyo kawaida, lakini kikubwa ilikuwa ni hamasa ya Watanzania hasa wakazi wa Dar es Salaam na vitongoji vyake, maelfu kwa maelfu kujipanga barabarani kumlaki kiongozi huyo katika njia zote alizopita kuanzia Uwanja wa Ndege.
Pamoja na mvua za masika zilizokuwa zinanyesha, hakuna aliyejali hali hiyo. Kila mmoja alikuwa na shauku ya kumwona Mandela.
Ilielezwa kuwa Mandela na ujumbe wake angewasili mapema zaidi, saa 4:00 asubuhi, lakini ratiba ilibadilika kuwa angewasili saa 11 jioni, lakini watu hawakupungua barabarani, walijipanga mapema kuanzia Uwanja wa Ndege, Barabara ya Pugu (sasa Nyerere) na maeneo mengine kumlaki mpigania uhuru huyo.
Wakati huo Dar es Salaam ilikuwa na tatizo kubwa la usafiri, lakini hakuna aliyejali. Mara baada ya Mandela kutua, ilinyesha mvua kubwa, watu walikubali kulowa lakini hadi wamwone Mandela.
Mandela alipata mapokezi makubwa na ya aina yake jijini Dar es Salaam. Kikubwa ni kwamba, Mandela alikuwa akizungumzwa sana na vyombo vya habari, kuonwa kwenye magazeti lakini wengi walitaka kumwona Mandela na mkewe Winnie uso kwa uso.
Baada ya shughuli za Uwanja wa Ndege kukamilika na mvua kukatika, Mandela aliyefuatana na mkewe, Winnie walipanda gari ya wazi aina ya Rolls Royce wakiwa na Mwalimu Nyerere kwa pembeni.
Maelfu kwa maelfu ya wakazi wa Dar es Salaam walijipanga kuanzia Uwanja wa Ndege, Barabara ya Pugu, Uhuru, Kariakoo, Stesheni, Luthuli hadi Ikulu na watu wote hao walikuwa na shauku ya kumuona Mandela walitimiza kiu yao. Kila mmoja alifurahi baada ya kumuona Mandela aliyekuwa akipunga mkono muda wote.
“Ndoto yangu imetimia”, “Siamini, nimemwona Mandela?”, “Safi”, “Naweza kufa kwa amani...nimemwona Mandela” zilikuwa kauli za watu mbalimbali waliokuwa wamejipanga barabarani kumlaki Mandela akiwa na Winnie walipokuwa wakipita.
Siku iliyofuata, hali ilikuwa zaidi ya siku ya mapokezi. Watu waliombwa kufika kwenye Uwanja wa Taifa (sasa Uwanja wa Uhuru) na ilikuwa mminyano wa aina yake. Zaidi ya watu 100,000 wanasadikiwa walifurika uwanjani kusikiliza hotuba ya pili ya Mandela tangu atoke gerezani.
Mandela alitoa hotuba ya kwanza akiwa City Hall nchini Afrika Kusini. Aliwahutubia wafuasi wa ANC wapatao 50,000 waliokuwa wakimsubiri kwa hamu kumuona baada ya kifungo cha miaka 27 jela, ambako pamoja na yote alionyesha furaha yake kulakiwa na maelfu ya wapenzi na wafuasi wake hao.
Mwalimu Nyerere akiwa na mgeni wake, alianza kumpongeza Mandela kwa kuwa ni kati ya watu wanaostahili heshima kutokana na mapambano yake dhidi ya siasa dhalimu ya makaburu wa Afrika Kusini. Makaburu walikithiri kwa siasa zao za kibaguzi.
Alisema kuwa kujitokeza kwa watu wengi kiasi hicho ilikuwa inadhihirisha kuwa Mandela anagusa akili za watu wengi kutokana na mapambano ya kumtetea mtu mweusi.
Kutokana na mchango wake wa kupigania haki na uhuru, Mwalimu Nyerere alimtunukia Mandela, Nishani ya Kilimanjaro Daraja la Pili ambayo mara nyingi hupewa Mawaziri Wakuu na viongozi wengine wenye kariba kama ya Mandela.
Akihutubia maelfu ya Watanzania na sauti yake nzito, Mandela alionyesha furaha yake kwa mapokezi makubwa ya Watanzania.
Pia Mandela alitumia nafasi hiyo kuwashukuru Watanzania kwa kukiunga mkono chama chake cha ANC katika mapambano ya ukombozi dhidi ya ubaguzi na utawala dhalimu wa makaburu.
Ziara ya Zanzibar
Machi 7, 1990 ujumbe wa Mandela ulikwenda Zanzibar ambako pia shughuli mbalimbali zikiwamo za biashara zilisimama kwa takribani saa nne, huku kila mmoja akiwa na shauku ya kumuona Mandela.
Mbali na kufurika mitaani, Uwanja wa Ndege ulikuwa umefurika pamoja na Uwanja wa Uwanja wa Amaan, Wazanzibar walijaa kumlaki ‘Comrade’ Mandela.
Neno ‘Amandla’ lilisikika kutoka kwa waliofika kumlaki Mandela aliyekuwa amepakizwa kwenye gari aina ya Landrover kwenda uwanjani.
Itakumbukwa, kwa mara ya kwanza, Mandela na Rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Karume, walikutana Addis Ababa mwaka 1962.
Mandela aliyetembelea Tanzania kwa mara ya kwanza katika ziara fupi mwaka 1962, alipofika Zanzibar baada ya kutoka gerezani, aliomba apelekwe kwenye Kaburi la Karume pamoja na eneo ambalo Rais Karume aliuawa.
Kati ya vitu alivyovizungumza akiwa Zanzibar, alisifu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na kwamba viongozi wa Afrika wanaosaka umoja, wajifunze muundo huo wa Muungano kutoka Tanzania.
Naye Winnie alisema kuwa atakaporudi Soweto atawasimulia Waafrika Kusini jinsi walivyopokewa vizuri, na kuwaeleza ukarimu walionao Watanzania.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment