Wednesday, 18 December 2013

NINI NI CHANZO CHA WIMBI LA UBAKAJI WATOTO TANZANIA? JE,NINI KIFANYIKE KUTOKOMEZA TATIZO HILI.

Na Anna Nindi, Stockholm, Sweden
Nimeona leo tuzungumzie swala la ubakaji. Hivi kwanini vitendo vya ubakaji vimekithiri sana kwa sasa nchini Tanzania?Nimevutwa na kuamua kuandika kuhusu swala hili baada ya jana kuangalia kipindi cha "RIPOTI MAALUM" kinachorushwa na kituo cha ITV.Kwanza kabisa napenda kuchukua nafasi hii kuwapongeza ITV kwa kazi nzuri wanayoifanya kwani ni wengi tulikuwa hatufahamu matatizo yanayowakabili watoto wetu.
 Mwandishi wa ITV Sam Mahela amefanya kazi nzuri sana kinachohitajika hapo ni vyombo husika kuchukua hatua zinazofaa haraka. 
Baada ya kuangalia kipindi cha "RIPOTI MAALUM"nilibaki na maswali mengi kuliko majibu.Je,hivi ni kwanini vitendo vya ubakaji kwa watoto vimekithiri kwasasa?Inachangiwa na ubutu wa sheria au kitu gani?
Je,sisi kama jamii tunajua kinachoendelea kuwakumba watoto? Kama ndiyo tunachukua hatua gani? Kama hatujui je,ni nani mwenye jukumu la kuielimisha jamii kuhusu ukatili huu?
Je,wizara husika imejenga mfumo gani katika kuhakikisha kuwa watoto wanayo njia rahisi ya kujieleza mara baada ya kufanyiwa ukatili wowote ikiwemo ubakaji?
Kuna mambo mengi ya kufanya hapa ili kumaliza hili tatizo na hakika inawezekana kabisa.Kwanza kabisa swala hili si la chombo kimoja.
NYUMBANI
Wazazi wawe karibu na watoto na wafuatilie kujua wanachofanya shule kila siku. 

SHULE
Walimu wanalo jukumu kubwa la kudadisi watoto vilevile kuhusu jinsi gani wanaishi na familia zao.Hii ni muhimu sana kwani baadhi ya watoto hutendewa ukatili majumbani kwao.
JAMII
Watoto wanapokuwa wakicheza iwe katika sehemu maalum za michezo au mitaani kwao ni jukumu la jamii nzima kuwalinda.Hii ni moja wapo ya haki ya msingi ya mtoto.
Kwa mfano katika kipindi nilichoangalia jana kuna mtoto mmoja alibakwa na mwanaume aliyemchukua chumbani kwake. Mtoto huyo aliambiwa na mwenzake waende wakacheze sehemu ambayo yeye huenda kucheza.
Sehemu aliyopelekwa kucheza ilikuwa  ni kwa mmbakaji huyo! Walipofika mwenzake aliaga kuwa anaondoka na mtoto aliyebakwa akamwambia mwenzie amsubiri achukue viatu waondoke wote.Alipokuwa akichukua viatu vyake ndipo mbakaji akamkamatwa na kumwingiza ndani na kumbaka.
Hapa ndipo linapokuja swala la jamii kutoa ushirikiano.Swali nililobaki nalo hapa ni je,mbakaji alikuwa anaishi nyumba ya kupanga au ya kwake? Je,alikuwa akiishi peke yake kiasi ambacho hakuna mtu aliyekuwa akishuhudia vitendo hivi? Kwani mtoto alisema mbakaji alishamfanyia kitendo hicho mara nne.Inasikitisha sana.
Nilimwonea huruma mama wa mtoto alivyokuwa akijieleza kwa uchungu jinsi anavyopata usumbufu polisi kufuatilia swala hili.
POLISI
Je,polisi wanachukua hatua inavyostahili kulingana na sheria inavyotaka?Mama aliyekuwa akihojiwa jana alilaumu ushirikiano hafifu alioupata kutoka kwa polisi.Polisi mjue ya kuwa na nyie mna watoto na huenda yakatokea kwa watoto wenu vilevile.Mama alilalamika kupewa majibu tofauti kila alipokwenda kituoni na kwa kifupi mtuhumia yupo uraiani  na labda anaendelea kuharibu watoto wengine.AIBU!
Naliomba jeshi la polisi msisaidie watu kulingana na uwezo waliokuwa nao kwani wengi wanaoathirika ni watu wa kipato cha chini kabisa.Fanyeni kazi kulingana na viapo vyenu na kwa kufuata sheria za nchi.Endapo askari huwezi kutimiza hivyo basi hiyo kazi umeingia ki makosa,acha katafute kazi inayokufaa.
Wito wangu kwa jamii :ni kwamba kila mmoja wetu awe mlinzi wa watoto.Hii itasaidia sana kuwabaini wahusika na kuwafikisha katika vyombo vya sheria.
Wito kwa wazazi: Muwape watoto malezi yanayostahili.Kwa wale watoto wanaofanyiwa ukatili na baba wa kambo wakina mama msiwatee waume zenu. Mama atakayefanya hivyo kwa kuficha ukatili aliofanyiwa mtoto naye apewe adhabu kama mmbakaji.
Wito kwa Wizara inayohusika ikishirikiana na taasisi zisizo za kiserikali iweke mfumo mzuri wa kupata taarifa za ukatili kwa watoto mara tu baada ya kutokea.Vilevile wizara husika ikishirikiana na wizara ya mambo ya ndani(polisi) wawe na kitengo binafsi kinachoshughulikia ukatili kwa watoto tu.
Mimi katika nchi ninayoishi mtoto anaheshimika sana na kusikilizwa.Mzazi unapokiuka majukumu yako serikali inakunyang´anya mtoto.Walimu wana jukumu kubwa katika malezi ya mtoto anapokuwa shuleni na endapo mtoto ataripoti kuhusu ukatili wowote anaofanyiwa nyumbani, walimu hupiga simu haraka kwa taasisi husika. Endapo itathibitika  kuwa ni kweli basi  mzazi/wazazi husika huchukuliwa hatua zinazostahili ikiwemo kunyang´anywa custody ya mtoto. 

Mwisho ningeomba kupata maoni mbalimbali kutoka kwa wadau kuwa nini zaidi kinaweza kufanyika kumaliza tatizo hili. Vile vile ningeomba kupata stori za ukweli kutoka kwa wale waliopatwa na tatizo hili  na madhara waliyoyapata ili tusaidiane.Tafadhali naomba watakaoniandikia wawe wahusika halisi (wazazi/walezi wa watoto ) na si vinginevyo.Tutafuatilia ukweli hivyo usiletee stori ya kutunga.
Taarifa zote muhimu ikiwemo majina tutafanya siri hivyo usihofu kuhusu usiri.
Asanteni

Unaweza kuniandikia kupitia: rainbowinfom@gmail.com


No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...