Friday, 20 December 2013

Usafiri Dar, Kanda Kaskazini balaa

Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra).
Hali ya usafiri katika Kituo Kikuu cha Mabasi yaendayo mikoani cha Ubungo (UBT) jijini Dar es Salaam, imezidi kuwa ngumu kutokana na baadhi ya mabasi yaendayo mikoa ya Kanda ya Kaskazini kuzaja hadi Desemba 25, mwaka huu.

Kanda ya Kaskazini inaundwa na mikoa ya Tanga, Arusha, Kilimanjaro na Manyara. 


Hata hivyo, mikoa ambayo usafiri wake ni mgumu kipindi hiki cha kuelekea katika sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya ni Kilimanjaro na Arusha.

NIPASHE lilipofika katika Kituo Kikuu cha Ubungo, lilishuhudia msongamano wa abiria wakigombea kupata tiketi ya kusafiri kwenda katika mapumziko ya Krismasi na Mwaka Mpya.

Msongamano huo uliwalazimisha watoa wauza tiketi wa kampuni kadhaa za mabasi kufunga milango ya ofisi zao na abiria kusimama nje ya ofisi hizo wakisubiri kufunguliwa bila mafanikio.

Mmoja wa wakala ambaye alijitambilisha kwa jina moja la Jimmy, alisema ofisi hizo zinakata tiketi kila baada ya siku mbili, hivyo tiketi za jana na leo tayari zimeuzwa na magari yamejaa.

“Tunakata tiketi siku mbili mbili, hivyo watakaokosa tiketi leo basi wajaribu kesho huenda wakabahatisha kupata japo sina uhakika,” alisema.

Wakati abiria wakisotea tiketi, hatua za kisheria zimeanza kuchukuliwa dhidi ya mabasi yanayotoza abiria nauli ya juu.

Jana alfajiri basi dogo aina ya Coaster inayofanya safari kutoka jijini Dar es Salaam kwenda mkoani Arusha ilikamatwa na kupigwa faini ya Sh. 250,000 kwa kosa kuwatoza abiria 38 nauli ya Sh. 40,000 badala ya Sh. 23,000.

Ofisa wa Chama cha Kutetea Haki za Abiria Tanzania (Chakuwa), Gervas Rutaguzinda, alisema waliamua kuchukua hatua hiyo kwa kushirikiana na Ofisa wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra).

Alisema pamoja na faini hiyo, abiria wote walirudishiwa kiasi kilichozidi na baada ya zoezi hilo likamilika safari iliendelea.

“Unajua kabla ya Chakuwa kuingia katika kituo hiki cha Ubungo, utapeli ulizidi sana, lakini hivi sasa tunaendelea kupambana nao, changamoto kubwa ipo kwa abiria kutojua haki zao kwa kushindwa kutoa ushirikiano kwa mamlaka zinazohusika,” alisema.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...