Wananchi wa Dumila mkoani Morogoro wakitumia uzoefu wao wa kuogelea kujinusuru na mafuriko yaliyotokea jana na kuhatarisha maisha ya watu wengi ikiwa ni pamoja na kuharibu madaraja.
Picha na Lilian Lucas
Morogoro. Mafuriko makubwa yametokea katika Kata ya Dumila, Kilosa mkoani Morogoro na kusababisha mamia ya watu kupoteza makazi huku daraja la Mto Mkundi linaloziunganisha Wilaya za Kilosa na Mvomero likivunjika.
Mafuriko hayo yalisababishwa na mvua kubwa zilizoanza kunyesha jana alfajiri na kusababisha maafa makubwa yakiwamo kuharibiwa kwa makazi ya watu, majengo ya Serikali zikiwamo shule, vyuo na mahakama.
Habari zinasema mafuriko hayo pia yalichangiwa na mvua kubwa iliyoanza kunyesha usiku wa kuamkia jana katika sehemu za milima iliyopo Kilosa na Mvomero, hivyo Mto Mkundi kushindwa kuhimili maji hayo.
Mashuhuda walisema waliona maiti ya mtu ikielea kwenye maji yaliyokuwa yakipita kwa kasi, tukio ambalo lilithibitishwa na Diwani wa Kata ya Magole, Juma Rajabu Chewe. Chewe alisema maiti hiyo ilionekana ikielea eneo la Mateteni na kwamba taarifa zilitolewa polisi ili aopolewe. Hadi jana jioni idadi ya watu walioathiriwa na maafa ilikuwa bado haijafahamika.
Maji yasambaa kwenye vijiji mbalimbali vinavyozunguka mto huo na kuwalazimisha baadhi ya watu kulazimika kujiokoa kwa kupanda kwenye paa za nyumba zao huku wengine wakikwea juu ya miti.
Baadhi ya watu walikutwa na mafuriko hayo mashambani na walipozidiwa na nguvu ya maji walijiokoa kwa kushikilia vitu mbalimbali ikiwamo miti, huku baadhi yao wakipoteza nguo walizokuwa wamevaa walipokuwa kwenye harakati za kujiokoa.
Polisi waliofika eneo hilo kwa ajili ya uokoaji walilazimika kuomba helikopta kutoka makao makuu ya jeshi hilo, Dar es Salaam ili kuwaokoa watu waliokuwa kwenye paa za nyumba na kwenye miti iliyokuwa imezungukwa na maji.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera alitaka kuwapo kwa uvumilivu wakati Serikali ikiendelea na taratibu za kuwaokoa walioko juu ya miti na kutoa misaada kwa walioathirika.
Alisema kuwa kutokana na hali kuwa mbaya, ofisi yake ililazimika kuomba helikopta kwa ajili ya kuongeza nguvu ya juhudi za uokoaji.
Taharuki kubwa
Mafuriko hayo yalizua taharuki kubwa kiasi cha wananchi kutawanyika ovyo wakiwa hawajui cha kufanya, kutokana na nyumba zao kuharibiwa na mali zao hususan mazao yakisombwa na maji.
Hali ilikuwa mbaya zaidi kwa kina mama wakiwa na watoto ambao walionekana katika makundi wakiomba msaada baada ya kukimbia makazi yao, huku wengi wakiwa wamelowa kutokana na kunyeshewa.
Mwanamke aliyejitambulisha kwa jina la Zahra Maulid alisema wanapata taabu na watoto kwani hawajui watakula nini baada ya mazao yao ukiwamo mpunga, mahindi na alizeti kusombwa na maji.
“Hapa hata hatujui tutaishi vipi maana vyakula vyetu vyote vimesombwa na maji, tunachoomba Serikali itupatie msaada wa haraka na mpaka sasa hatujui mlo wetu wa leo na hata wengine hawana makazi,”alisema Zahra.
Habari zaidi kutoka Dumila zilisema, madarasa ya Shule ya Msingi Magole, nayo yalifunikwa na maji na wanafunzi waliokuwamo walijiokoa kupita madirishani.
Majengo ya Shule ya Sekondari ya Wasichana Dakawa, Chuo cha Veta Dakawa na Mahakama ya Mwanzo Dakawa nayo yaliharibiwa na mafuriko hayo.
Wanafunzi wa Sekondari ya Dakawa walikuwa nje ya mabweni wakisubiri maji kukauka. Majalada ya kesi mbalimbali katika Mahakama ya Mwanzo Dumila yalilowa maji, huku tope zito likionekana ndani ya chumba cha mahakama hiyo.
Mafuriko hayo pia yalisababisha kusombwa kwa nguzo za umeme na kufungwa kwa barabara nyingine kadhaa kutokana na miti mikubwa kukatika na kutanda katika barabarani hizo.
Pia vituo 11 vya treni vilivyoko mkoani Morogoro vimeathirika kutokana na mafuriko baada ya kusombwa na maji.
Magari yakwama
Magari zaidi ya 5,000 yaliyokuwa yakitokea Dar es Salaam, Tanga na Pwani kuelekea Bara na yale yaliyokuwa yakitokea Bara kwenda Dar es Salaam yalikwama huku, mengine yakigeuza na kurejea yalikotoka.
Abiria aliyekuwa katika moja ya mabasi yaliyokwama, Godfrey Wambura alilalamikia kukosekana kwa huduma za kijamii katika eneo hilo na kwamba bidhaa muhimu zilikuwa zimeanza kuuzwa kwa bei ghali. Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk Charles Tizeba ambaye alifika mapema kwenye eneo hilo, alishauri magari yaliyotokea yanatokea upande wa barabara kurudi Dodoma na kwenda Iringa kwa ajili ya kuja Dar es Salaam.
Meneja wa Wakala wa Barabara (Tanroads) wa Mkoa wa Morogoro, Doroth Mtanga alisema haifahamiki ni hasara gani iliyotokana na kuvunjika kwa daraja hilo.
Wakati huohuo, jana Serikali ilitangaza kufunga Barabara ya Morogoro – Dodoma kuanzia jana, na kuwashauri wale wenye safari za lazima kutumia barabara mbadala kwani eneo la Dumila halipitiki.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi aliliambia gazeti hili jana jioni kuwa: “Magari yanayoendelea kutumia barabara hiyo yanaweza kusababisha maafa zaidi maana eneo hilo halipitiki, lakini kibaya zaidi Kijiji cha Dumila ni kidogo, hakiwezi kuhimili idadi ya watu wote waliokwama na watakaokwama.”
Aliongeza: “Magari yanayotoka Dar es Salaam yapitie Chalinze – Arusha – Babati - Singida – Mwanza na yale yanayotoka Mbeya yatumie Barabara ya Iringa – Dodoma – Arusha – Kondoa kuelekea Arusha au Mwanza.”
Alisema mafundi wameanza kazi ya kurejesha hali ya kawaida katika daraja lililobomoka na kwamba barabara hiyo imefungwa kuanzia jana na itaendelea kufungwa leo, huku akiwashauri madereva wa magari yaliyoko katika eneo hilo waondoke na kurejea yalikotoka.
Kuhusu waliopatwa na maafa, waziri huyo alisema Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Morogoro ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa, Joel Bendera ilikuwa eneo la tukio kufanya tathmini ya maafa hayo.
“Hapa kwetu tumekusanya mahitaji ya chakula, mablanketi, mahema na vyote hivyo vinaondoka jioni hii (jana) kwa gari la jeshi kwenda eneo la maafa,” alisema Lukuvi.
CHANZO:MWANANCHI
No comments:
Post a Comment