Tuesday 7 January 2014

MTU HUYU ANAHITAJI MSAADA.NI FRANCIS BENARD; MIAKA 29 KITANDANI MUHIMBILI, HANA NDUGU!

ALIPOPANDA basi kutoka Tanga kuelekea Dar es Salaam mwezi fulani mwaka 1984, hakujua kama ilikuwa ni siku yake ya mwisho kuwa mzima, mwenye mwili mkakamavu uliokamilika viungo vyote.


Akiwaacha nyuma mkewe, Veneranda Makamba na watoto wake wawili, Bashangi (aliyekuwa na umri wa miaka 12) na James (10), Francis Benard aliyekuwa na umri wa miaka 46 wakati huo, uzima wake ulikomea maeneo ya Mto Wami, ambako alipata ajali iliyomlaza kitandani akiwa mahututi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa miaka sita.
Hadi wakati akipata ajali hiyo, Francis alikuwa mjasiriamali, hivyo tukio hilo liliharibu kabisa mfumo mzima wa maisha yake kiuchumi.
Na bahati mbaya nyingine, akiwa hospitalini hapo, mkewe Veneranda alifariki dunia na hivyo kusababisha watoto wake kulelewa na watu asiowafahamu hadi leo akiwa na umri wa miaka 75.
Mzee Francis amepooza sehemu kubwa ya mwili wake, hali inayomfanya awe mtu wa kulala tu na akibadilisha sana ‘style’ basi ni kukaa. Hawezi kusimama, hawezi kutembea na hana hata ndugu. Kwa miaka 29 sasa anaishi na watu asiowafahamu.
Baada ya kukaa kwa miaka mingi hospitalini hapo akiwa katika hali hiyo, ambayo mwenyewe aliielezea kama kupata nafuu, alihamishwa na kupelekwa katika kituo cha kuhudumia watu wasiojiweza kinachojulikana kama Kwa Mama Theresa, kilichopo Mburahati jijini Dar es Salaam.
“Nikiwa nimelazwa pale Muhimbili, nilijifunza kufuma maua na vitambaa kiasi kwamba baadhi ya wagonjwa wenzangu wakanitambua. Wakawa wanakuja kwangu wananunua. Hadi napelekwa Mburahati nilishakuwa maarufu na nikawa na wateja wengi.
“Sasa nilipohamishiwa kule, wateja wangu wakawa wanaendelea kunifuata, kitendo kile kikawaudhi baadhi ya wenzangu wa pale, wakaanza kuninunia, wakawa wananinyima baadhi ya vitu,” anasema mzee Francis.
Baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya kwa upande wake, alisema aliamua kukodi teksi kwa fedha kidogo alizozihifadhi na kuelekea Muhimbili ambako alipewa tena kitanda hadi sasa.
Anawashukuru sana wauguzi na uongozi wa hospitali hiyo ya taifa, kwani wanamtunza vizuri, licha ya taabu kubwa ya kimwili anayoipata.
Mzee Francis yupo wodi namba 14 katika Jengo la Kibasila na kidogo kidogo bado anaendelea kujikimu kwa namna hiyo ya kufuma na kutengeneza maua, ambayo pia yamemfanya kupata marafiki.
MSAADA
Kutokana na uwezo wake wa kujua kufuma vitambaa na kutengeneza mapambo mengine ya urembo, mzee huyo anaomba kuwezeshwa zaidi ili aweze kujiongezea kipato.
Na kwa vile ajali hiyo ilimfanya ashindwe kusimama wala kutembea, anamuomba Mtanzania yeyote kumsaidia baiskeli ya walemavu ili aweze kutembelea ambayo alisema amesikia kuwa zinauzwa shilingi laki nane za Kitanzania.
Kwa aliyeguswa na tatizo la mzee huyu anaweza kwenda Hospitali ya Muhimbili wodi 14 Kibasila au kuwasiliana naye moja kwa moja kupitia simu yake namba 0653313804.
CHANZO: GPL

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...