Friday 3 January 2014

MWILI WA MGIMWA KULETWA KESHO,JOMBONI WAMLILIA


Dk. William Mgimwa

Kuzikwa Iringa Jumatatu

Mwili wa aliyekuwa Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa, unatarajiwa kuwasili Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Nyerere kutokea Afrika Kusini kesho.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya mazishi hayo kitaifa, aliyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.

Alisema mwili wa marehemu utawasili na ndege ya Shirika la Ndege la Afrika Kusini wakati wa mchana na kupelekwa moja kwa moja nyumbani kwake Mikocheni B na baadaye jioni utapelekwa katika Hospitali ya Jeshi Lugalo kwa ajili ya kuhifadhiwa.

Jumapili saa nne na nusu asubuhi mwili huo utapelekwa nyumbani kwake na baadaye utapelekwa katika ukumbi wa Karimjee, kwa ajili ya kutolewa heshima za mwisho.

“Wananchi wote watakaoshindwa kusafiri kwenda Iringa watapata nafasi ya kutoa heshima zao za mwisho katika ukumbi wa Karimjee, hivyo wananchi mnaombwa kufika eneo hilo,” alisema Lukuvi.

Alisema alasiri mwili wa marehemu utapelekwa Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Nyerere kwa safari ya kuelekea mkoani Iringa.

Lukuvi alisema kuwa majira ya saa 10 alasiri mwili utawasili Uwanja wa Ndege wa Iringa baadaye kuagwa katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo uliopo mkoani humo.
Alisema Jumapili saa 11:30 jioni mwili wa marehemu Mgimwa utasafirishwa kuelekea kijijini kwake Magunga, na Jumatatu mchana shughuli za mazishi zitafanyika katika kijiji hicho.

Alifafanua kuwa serikali imeunda kamati kwa ajili ya kushughulikia msiba huo kuanzia kuwasili kwa mwili uwanja wa ndege hadi siku ya mazishi kijijini kwake.

Alisema kamati hiyo inayoongozwa na yeye, ikiwa na wajumbe kutoka Wizara ya Fedha, Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Afya, Bunge, Ikulu, na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Alisema mbali na kuwapo kwa kamati hiyo, pia kumeundwa kamati nyingine ndogo ya mkoa wa Iringa inayoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma.

“Hivyo kwa wakazi wa Iringa, marafiki zake na jamaa wa karibu watapata nafasi ya kuuaga mwili wa marehemu katika ukumbi huo, shughuli zitakazoongozwa na kamati ndogo ya Iringa,” alisema Lukuvi.

Lukuvi alisema kuhusu sababu iliyosababisha kifo cha marehemu Mgimwa itaelezwa siku ya kuuaga mwili katika ukumbi wa Karimjee.

“Hatuwezi kuficha sababu ya kifo chake, hata hivyo, mwili ukifika uwanja wa ndege utakuja na death certificate (hati ya kifo), hivyo kuweni na subira na muweke akiba ya habari,” alisema Lukuvi.

JIMBONI KALENGA WAMLILIA
Wakati huo huo, wakazi wa Jimbo la Kalenga, wilaya ya Iringa vijijini, mkoani Iringa, wamesema kifo cha mbunge wao, Waziri, Dk. Mgimwa, kimeacha pengo kubwa kwa kuwa aliwathamini na kutatua matatizo yao kwa wakati.

Wakizungumza na NIPASHE kwa nyakati tofauti, Raphael Lengesia, alisema baada ya kusikia taarifa ya kuhusu kifo cha mbunge wao alipata mshtuko kwa kuwa ni pengo ambalo halitazibika kwao.

“Sisi kama wakazi wa jimbo hili, tumesikitika sana kupata taarifa hizi ambazo zimemgusa kila mmoja wetu kutokana pengo hili ambalo ametuachia, tulikuwa tukiuthamini mchango wake katika kutusaidia kutatua matatizo yetu wakati akiwa jimboni,” alisema Lengesia.

Maimuna Nzigiwa, mkazi wa Ifunda, alisema mbali na kuwa na majukumu ya kitaifa, Dk. Mgimwa aliwatumikia wapiga kura wake kwa uaminifu na bidii kubwa.

“Hatuna hakika kama tutapata kiongozi mwenye busara kututetea wananchi hasa wa vijijini kulingana mambo mengi aliyoyafanya hapa kijijini kwetu,” alisema Nzigiwa.
Aliongeza kuwa, marehemu alikuwa akiwapigania kwenye masuala mbalimbali ikiwamo barabara, shule, zahanati hususan maji na kuwawezesha kupata maji na kwamba wataendelea kumkumbuka. 

Ramadhan Salehe, alisema mchango wa Dk. Mgimwa ulikuwa mkubwa na kuwataka viongozi wengine kuiga ili kuwa na maendeleo endelevu.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Iringa, Steven Mhapa, alisema ni pigo kubwa kutokana na mchango wa marehemu katika kuisaidia jamii na kuwa imepoteza mtu mwenye busara na mchapakazi, ambaye alishirikiana na halmashauri hiyo katika kuwatafutia wafadhili kwa ajili ya kutatua changamoto mbalimbali za kimaendeleo.

MTOTO WAKE AZUNGUMZA
Akizungumza na NIPASHE, nyumbani kwao Mikocheni B jana, mtoto wa marehemu, Godfrey Mgimwa, alisema baba yake enzi za uhai wake alikuwa ni mtu wa dini na kwa jinsi hiyo aliwalea katika misingi ya maadili ya kidini, na kwa kifo chake wamempoteza mzazi aliyekuwa wa umuhimu sana kwao.

Alisema, baba yake pia hakuwa mtu mbinafsi kwani aliwasaidia watu wengi wakiwamo wa jimboni kwake.

Kuhusu idadi ya watoto, Godfrey alisema, baba yake amemwacha mama yake ambaye amekuwa akimuuguza nchini Afrika Kusini, watoto wa kike wawili na wa kiume kadhaa, kwani idadi kamili ya watoto alioacha marehermu baba yake ni siri yao.

Kwa mujibu wa Godfrey, baba yake alikuwa mtu aliyependa familia yake, kwani hakuwa mwepesi kuwapa mali ovyo bila sababu za msingi hata kama alikuwa ni mtu mwenye nafasi kubwa serikalini.

Baadhi ya viongozi wa serikali ambao hadi jana walikuwa wamefika nyumbani hapo kwa ajili ya kutoa pole, ni pamoja na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi; Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Yusufu Mwenda na Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Adam Malima.

Wengine ni manaibu mawaziri wa Fedha, Janet Mbene na Saada Mkuya; Mbunge wa Namtumbo, Vita Kawawa na baadhi ya viongozi wengine wa vyama vya siasa. 

Imeandikwa na Gwamaka Alipipi, Isaya Kisimbilu, Dar na George Tarimo, Iringa. 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...