Saturday, 18 January 2014

Rais Kikwete aozesha mwanaye

kikwete+clip[1]
Miraji Kikwete na Aima Mahmoud wakiondoka kwenye ukumbi wa Mlimani City baada ya kufunga ndoa yao jana. Picha na Florence Majani 

Shamra shamra na nderemo zilitawala jana kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Mlimani City wakati Miraji Kikwete, mtoto wa Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete alipofunga ndoa na Alma Mahmoud.
Sherehe hizo zilianza saa 7:00 mchana baada ya ndoa kufungwa na maharusi hao kuingia ukumbini hapo wakiongozana na Rais Kikwete.
Hali nje ya ukumbi huo ilikuwa tulivu ingawa uwanja ulikuwa umefurika magari ya polisi, viongozi na wageni waalikwa. Huku kikosi cha kudhibiti ulinzi na usalama kikiwa kimefunga mitambo ndani na nje ya ukumbi huo.
Ulinzi katika eneo hilo ulikuwa ni mkali kupita kiasi ambapo hakuna yeyote aliyeruhusiwa kuingia ukumbini humo bila kadi maalumu, hata angeomba kwa kupiga magoti.
“Hata sisi tumetoka Bagamoyo hadi hapa tuna undugu kabisa na mkubwa (Rais Kikwete), lakini wametunyima kwa sababu hatuna kadi,” alilalamika mwanamke mmoja aliyeongozana na wanaume wawili.
Hakuna waandishi wa habari walioruhusiwa kuingia ndani ya ukumbi huo, isipokuwa waandishi na wapiga picha maalumu wa Serikali ambao walipewa vitambulisho maalumu na tisheti.
Wengine walioonekana wakipiga picha ni wanafamilia ambapo watoto wa kiume wa Rais Kikwete, walionekana wakiwa na kamera huku wamevalia kanzu nadhifu.
Mfanyakazi mmoja wa Ikulu alipomwona Mwandishi wa gazeti hili, alimfuata na kumwambia kuwa sherehe hiyo ni ya kibinafsi na haruhusiwi mwandishi yeyote kufanya kitu chochote.
“Tumenyimwa kuruhusu waandishi kwenye sherehe hii, sawa wewe ni mwandishi lakini hii ni sherehe binafsi na ya kifamilia, huruhusiwi kupiga picha yeyote,” alisema mfanyakazi huyo, jina linahifadhiwa.
Hata hivyo, mwandishi alitumia mbinu kupata picha za maharusi hao pamoja na matukio mengine yaliyokuwa yakiendelea ukumbini hapo.
Wageni wengi waalikwa walianza kuingia ukumbini humo majira ya mchana na wengine waliendelea kuwasili hadi saa 11 za jioni.
Miongoni mwa viongozi wa kitaifa waliohudhuria sherehe hizo ni pamoja na Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal, Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, Waziri wa Afya, Dk Hussein Mwinyi, Naibu Waziri wa Afya, Dk Seif Rashid na Waziri wa Maendeleo ya Wanawake Jinsia na Watoto, Sophia Simba.
Wengine waliokuwepo ni Mkuu wa Jeshi la Polisi Mstaafu, Inspekta Jenerali Omari Mahita, Mkurugenzi wa Mashindano ya Urembo ya Miss Tanzania, Hashim Lundenga, Sheikh Mkuu wa Tanzania Mufti Issa Shaaban Simba na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadicky.
Muda wa chakula ulianza mida ya saa kumi jioni ambapo baada ya bwana na bibi harusi kuchukua chakula, wageni waalikwa nao walianza kuitwa kwa makundi na kwa ustaarabu wa hali ya juu kuchukua chakula.
Hata hivyo kutokana na wingi wa watu waliofurika ukumbini hapo, msururu wa chakula haukumalizika hadi Miraji na mke wake mpya wanaondoka ukumbini hapo.
Rais Kikwete ambaye alikuwepo katika sherehe hiyo alikuwa wa kwanza kuondoka ukumbini hapo muda wa saa 11:30 jioni akifuatiwa na Rais Mwinyi na viongozi wengine wa kitaifa.
Maharusi walikuwa wa mwisho kutoka ukumbini baada ya viongozi wote wa kitaifa kuondoka huku wimbo maarufu wa “Aiya iyaaa kuolewa utarudi nyumbani kutembea” ukiwasindikiza jambo ambalo bila shaka lilimuumiza bibi harusi huyo ambaye alianza kulia huku Miraji akionekana kumbembeleza.
Baada ya Alma kuingia kwenye gari, Miraji naye aliingia akiwa anacheza kwa furaha huku Ridhwani akimfungulia mlango.
CHANZO: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...