Friday, 31 January 2014

TIBA MBADALA: Kunywa maji ya moto ni tiba ya magonjwa mengi


Kwa mujibu wa wataalamu wa afya maji moto yanatibu magonjwa mengi ikiwemo: Figo, kutoa sumu mwilini, kuyeyusha mafuta tumboni, kurahisisha mzunguko wa damu, kuondoa sumu kwenye ubongo na kusafisha haja ndogo. 
Kuna tiba nyingi za kitabibu, zilizogawanyikaa katika makundi mbalimbali. Kuna zile za hospitali ambazo ni lazima zinunuliwe, lakini kuna tiba ambazo kwa ushauri wa daktari hata wewe unaweza kuziandaa bila kutumia gharama kubwa.
Moja ya tiba hizo ni kunywa maji ya moto. Kwa mujibu wa wataalamu wa afya maji moto yanatibu magonjwa mengi ikiwemo: Figo, kutoa sumu mwilini, kuyeyusha mafuta tumboni, kurahisisha mzunguko wa damu, kuondoa sumu kwenye ubongo na kusafisha haja ndogo.
Kunywa maji ya moto kila unapotaka kwenda kufanya kazi ya nguvu au mazoezi iwe kamakinga na inashauriwa kila siku anywe glasi nane ili kutoa taka na kila kisichotakiwa kubaki mwilini, kupitia jasho.
 Wadau wa afya wanasema kuwa  ni vyema pia kunywa maji ya moto yenye ndimu au limao kabla ya kifungua kinywa ili kurahisisha mfumo wa mwili kwa siku nzima.
Pazi Mwinyimvua,  Mtaalamu wa Chakula na Lishe kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, anasema kuwa maji yanarahisisha uyeyushaji wa chakula na mafuta mwilini, hivyo kutokana na umuhimu huo ni vyema kunywa maji  ya moto yatakayofanya kazi haraka na kwa ufanisi mkubwa bila kuchosha figo.
Anaitaja faida nyingine ya kunywa maji ya moto kuwa ni kutoa sumu zilizopo kwenye mishipa ya fahamu na kuisaidia figo kufanya kazi kikamilifu, tofauti na maji baridi ambayo yanagandisha na kuilazimisha figo kuyeyusha kwanza na kisha kuchuja
Anashauri umuhimu wa kunywa maji moto kabla ya kufanya mazoezi kuwa ni kujiandaa kwa ajili ya kuchuja jasho ambalo litatoa sumu, hivyo yakiwa ya moto yakifika yanaanza kufanya kazi moja kwa moja, kuliko yakiwa ya baridi yanaweza kusumbua kwa kuwa ni lazima yapate joto la mwili kwanza kabla ya kuanza kufanya kazi.
“Ukiachilia kusubiri yachemke pia ni kumuepusha mtumiaji na hatari ya kuumwa tumbo kutokana na kunywa maji ya baridi bila kuweka kitu tumboni na kwenda kufanya mazoezi kitu kinachoweza kuzidisha maumivu au maji kucheza wakati wa kukimbia kama mazoezi ya kukimbia. Lakini yakiwa ya moto ni kama umekunywa chai au kula chakula cha kawaida” anasema Mwinyimvua.
Mwinyimvua anaongeza kuwa maji ya moto ni mazuri hata kwa kupata choo, kwa vile kinarahisisha uyeyushaji na uchambuaji wa kinachotakiwa na kisichotakiwa, wanaokunywa ya baridi wana uwezekanao mkubwa wa kupata haja kubwa kwa shida.
Vilevile Mwinyimvua anashauri kuwa ni vyema kunywa maji moto yaliyochemshwa na kuyaacha yapoe na kuwa vuguvugu na kuongeza limao na asali  mbali na kuongeza  ladha, asali na limao vina faida kiafya.
Gayl Canfield , RD, Mkurugenzi wa Lishe kutoka katika Kituo cha Biashara cha Pritikin Longevity kwenye Mji wa  Miami , Florida nchini Marekani, anasema kuwa kunywa maji ya uvuguvugu au ya moto ni vyema kwa kuwa hufanya kazi moja kwa moja kutokana na hali ya tumbo kuwa na joto muda wote.
Canfield anasisitiza, “Maji ni muhimu kwa mwili wako,  yakiwa ya   moto ni bora zaidi, kwa kuwa yanatoa rangi ya njano ya mkojo na kuufanya uwe msafi na wenye rangi angavu”.
Anasema  maji ya moto yanaweza kukusaidia kupoteza uzito au kudumisha uzito ulionao sasa.
 “Maji ya moto yanaweza  kuongeza joto la mwili na hivyo kuongeza kiwango  ufanyaji kazi wa mwili kidogo, “ anasema Dk Michael Wald , Mkurugenzi wa Huduma za lishe katika kituo cha Integrated kilichopo  New York, Marekani.
Anasema  ili mwili ufanye kazi ipasavyo husaidia utumbo na figo kufanya kazi kwa ufanisi zaidi. Kunywa maji ya moto pia husaidia kupunguza uzito wa mwili na  kuwa na  nuru na siyo kusinyaa. Vilevile huchangamsha utendaji kazi wa ubongo.
Dk  Michael Wald anaitaja faida  nyingine ya kunywa maji ya moto kuwa ni kujenga mazoea ya kuchemsha maji hivyo kupunguza idadi ya maambukizi yanayotokana na kunywa maji bila kuchemsha.
“Maji baridi hugandisha mafuta ndani ya miili yetu, ikiwa ni pamoja na mishipa ya damu,hali hii ikiendelea inaweza kusababisha  shinikizo la damu kutokana na ukosefu wa mzunguko wa damu pamoja na magonjwa mengine mengi. Kama haikufanyiwa kazi  inaweza hata kusababisha saratani ” anasema Dr Michael Wald .
Mganga Mkuu Hospitali ya Amana, Dk. Meshack Shimwela, anasema kuwa kunywa maji ni muhimu yawe  baridi au ya moto na hakuna sababu za kitaalamu zinazohusisha na dawa au kutibu kitu chochote.
Anasema, watu wa tiba mbadala ndiyo wamelikuza hilo lakini kitaalamu halipo na kunywa maji ni muhimu kwa kila mtu bila kujali ni ya moto au baridi, hayo mengine ni maneno tu.
“Watu wanashauriwa kunywa maji ya moto kwa wale wasiopenda kunywa maji, kwa kuwa yakiwa ya uvuguvugu inakuwa nafuu kwao kunywa na wengine huambiwa waweke ndimu au limao siyo kama dawa bali kuyapa ladha ili waweze kunywa” anasema Shimwela.
Anaendelea kufafanua kuwa kama kuna wanaodharau kunywa maji wakiona ni kitu kidogo wanakosea sana kwa kuwa maji ni msaada hata unapopata tatizo la kiafya.
Anasema kuwa hata katika usagaji wa chakula maji husaidia, hivyo kama mhusika amekunywa maji atarahisisha kitendo hicho.
Dk Raymond Mwenesano wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, anasema kuwa kunywa maji ni muhimu kwa kila mwanadamu ili kurahisisha utendaji wa mwili ikiwamo mzunguko wa damu bila kujali ni moto au baridi.
Dk Mwenesano anazitaja faida za kunywa maji moto kuwa ni : Kuboresha uyeyushwaji wa chakula. Maji ya vuguvugu yakiwekwa limao, yanasaidia usafishaji wa tumbo, kuondoa sumu mwilini kupitia jasho, kusafisha pua na koo, kuboresha mzunguko wa damu , husaidia upatikanaji wa haja kubwa, kuongeza kinga mwilini endapo asali na limao vitaongezwa.
CHANZO: Mwananchi

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...