Dar es Salaam. Waumini mbalimbali wa dini ya Kiislamu nchini, wanaungana na wenzao duniani kote leo katika mapumziko ya kuadhimisha Sikukuu ya Maulid ikiwa ni kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (SAW) miaka 1345 iliyopita.
Msemaji wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Shaaban Simba alisema jana kuwa, kitaifa Maulid hayo yalifanyika jana usiku mkoani Kigoma.
Alisema Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Issa Bin Shaaban Simba ndiye aliyeongoza Maulid hayo kitaifa na mgeni rasmi alitarajiwa kuwa Mkuu wa mkoa huo, Issa Machibya.
Simba alitumia fursa hiyo kuwatakiwa Watanzania wote mapumziko mema ya Maulid kwa kusherehekea kwa amani na kuepuka kujihusisha na vitendo viovu.
“Tunawaomba wananchi kutumia mapumziko haya vizuri kwa lengo la kulinda amani na utulivu wa nchi yetu,” alisema Simba. Jijini Dar es Salaam, maadhimisho hayo yalifanyika kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja na mgeni rasmi alitarajiwa kuwa Rais Mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi.
CHANZO: MWANANCHI
RAINBOW-TZ inawatakia waislamu wote mapumziko mema ya sikukuu hii ya maulid
No comments:
Post a Comment