Monday, 17 February 2014

Asilimia 70 wamefungwa Jela kwa kutozijua sheria

Mtandao wa watoa huduma wa msaada
 wa kisheria nchini (TANLAP).
Imeelezwa kuwa asilimia 70 ya wafungwa waliomo katika magereza nchini wamefungwa kutokana na kutokuzijua vizuri sheria za nchi na haki zao za msingi.

Hayo yalibainishwa  wakati wa mafunzo ya siku nne ya kuwajengea uwezo viongozi wa asasi zinazojishughulisha na utoaji wa huduma ya msaada wa kisheria mkoani Shinyanga yaliyoendeshwa na Mtandao wa watoa huduma wa msaada wa kisheria nchini (TANLAP).

Ilielezwa kuwa watu wengi hupoteza haki zao za msingi katika mahakama mbalimbali kutokana na kutozijua vyema sheria za nchi kutokana na kushindwa kujitetea vizuri, hivyo kuhitajika juhudi za kuielimisha jamii ili kutambua haki zao za msingi na sheria.


Mmoja wa wawezeshaji wa mafunzo hayo, Edna Bakebwa ambaye ni mwanasheria wa kutoka TANLAP, alisema utafiti uliofanywa hivi karibuni umebaini asilimia 70 ya watu waliomo ndani ya magereza walitiwa hatiani kutokana na kutozijua vyema sheria za nchi.

Bakebwa alisema kutokana na hali hiyo, kuna kila sababu kwa watoa huduma za msaada wa kisheria kujikita katika kuielimisha jamii ili kuzifahamu baadhi ya sheria muhimu na mambo wanayostahili kutendewa pale wanapofikishwa mahakamani au wao wenyewe kufungua mashitaka.

Alisema watoa huduma za msaada wa kisheria wanayo fursa ya kuwatembelea wafungwa waliomo magerezani na kuelimishwa juu ya haki zao za msingi kwa mujibu wa katiba ya nchi na kwamba kwa wale wanaofikishwa katika vituo vya polisi wanayo haki ya kutoa maelezo yao mbele ya mtu au wakili wanayemtaka.

Alisema siyo tabia nzuri ya watoa huduma za msaada wa kisheria kukaa bila ya kuielimisha jamii juu ya haki zao za msingi na kusubiri mpaka pale wanapopatwa na matatizo ndipo hujitokeza kwenda mahakamani kuwapatia msaada wa kisheria.

Katika hatua nyingine washiriki wa mafunzo hayo waliwaomba wabunge wa Bunge la Katiba kuhakikisha wanajadili rasimu ya pili ya mapendekezo ya katiba mpya bila ya kutanguliza maslahi ya vyama vyao vya kisiasa na kwamba watangulize mbele uzalendo.

“Tunawaomba wawe makini katika mjadala mzima wa rasimu ya katiba, watakapoingia ndani ya ukumbi wa bunge waache mlangoni itikadi na mapenzi ya vyama vyao vya siasa, waheshimu mapendekezo yaliyopendekezwa na Watanzania, hasa katika suala la haki za binadamu lizingatiwe sana,” alieleza John Shija kutoka PACESHI.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...