Mtoto Pendo Sengelema akiwa amelazwa katika Hospitali ya Urambo baada ya kukatwa mkono wa kulia na watu wasiojulikana. Picha na Robert Kakwesi
Urambo. Mganga mmoja wa kienyeji na jirani wa binti, Pendo Sengerema (15), anashikiliwa na polisi kwa kuwaonyesha wahalifu anakoishi mtoto huyo mwenye ulemavu wa ngozi (albino), ambao walimkata mkono na kuondoka nao.
Mganga huyo anadaiwa kuwaeleza polisi kuwa alishawishiwa na watu hao kwa ahadi ya kupewa Sh900,000 na alitanguliziwa Sh200,000.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Salome Kaganda alisema ataeleza zaidi kuhusu tukio hilo leo.
Mtu huyo anayeishi umbali wa takriban nusu kilomita kutoka anakoishi msichana huyo, anataka watu waliomkata mkono Pendo wakamatwe kwa sababu anawadai.
Mkuu wa Wilaya ya Kaliua ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Urambo, Saveli Maketa alikwenda kumtembelea Pendo na kuzungumzia kukamatwa kwa mtu huyo.
Mwenyekiti wa Shirikisho la Watu wenye Ulemavu Wilaya za Urambo na Kaliua, Daniel Mwita licha ya kulaani tukio hilo, alitaka jamii kuwa walinzi wa watu wenye ulemavu badala ya kuwaangamiza.
“Wananchi wanaoishi na watu wenye ulemavu wa ngozi, lazima wawe askari wa mstari wa mbele kuwalinda ili wasidhuriwe,” alisema.
Mratibu wa Chama cha Albino, Tawi la Urambo na Kaliua, Focus Magwesela alimwomba Rais Jakaya Kikwete kusisitiza wananchi kuwa maisha mazuri au utajiri haupatikani kwa imani za ushirikina.
Alisema viongozi wote wa vyama vya watu wenye ulemavu watalifuatilia suala hilo na kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola ili haki itendeke kwa wahusika.
CHANZO: MWANANCHI
ANGALIZO: Tumetoa habari hii kwani ili tuushinde ukatili huu kila mwananchi anatakiwa awe mlinzi wa watu wenye ulemavu wa ngozi. Kila binadamu ana haki ya kuishi.
Pamoja inawezekana.
No comments:
Post a Comment