Zaidi ya Sh bilioni 14 zimebadilishwa kupitia huduma ya Dawati la China katika benki ya CRDB ili kuwawezesha wafanyabiashara wa nchini Tanzania kupata fedha kwa ajili ya kununua bidhaa nyingine nchini China.
Hayo yalisemwa na Meneja Mahusiano anayesimamia dawati la China kutoka CRDB, Ibrahim Masahi, wakati wa Maonyesho ya Biashara ya China, yaliyofanyika Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam, ambapo alisema kuwa tangu kuanzishwa kwa huduma hiyo wafanyabiashara wengi wamefanikiwa.
Masahi alisema, huduma hiyo imepata ongezeko la asilimia 70 ya wateja ambao ni Watanzania wanaokwenda China ama wachina wanaokuja Tanzania kwa ajili ya shughuli za biashara au matembezi.
Alisema kupitia dawati hilo, kuna huduma ya Union Card ambayo ni sawa na Master Card au Visa Card zinazomwezesha mteja kutoka Tanzania kuchukua fedha kwenye ITM ya benki yoyote akiwa nchini China na kufanya biashara pale anapokuwa fedha zimemuishia.
Masahi alisema ili kuboresha huduma hiyo ya Dawati la China, CRDB imeweka mahusiano ya kibishara na Benki mbili nchini China ambazo ni Bank ya China HBC ya Beijing nchini huko kwa ajili ya huduma ya kusafirisha fedha kwa haraka zaidi kutoka Tanzania.
Alisema lengo la kuanzishwa kwa huduma hiyo ni kuwasaidia wafanyabiashara kuweza kutoa fedha wakiwa nchini China na kuendelea kuongeza bidhaa zao kwa ajili ya kukuza uchumi wa Tanzania .
Maonyesho hayo yalifunguliwa juzi na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, ambayo zaidi ya kampuni 100 kutoka China zinaonyesha bidhaa mbalimbali zikiwemo za nyumbani pamoja na za kiteknolojia.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment