Chupi za Mitumba
Msako mkali wa kuwabaini na kuwakamata waagizaji, wasambazaji na wauzaji wa nguo za ndani (chupi) za mitumba unatarajiwa kuanza wiki ijayo nchi nzima.
Hatua hiyo imefikiwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) baada ya kuona nguo hizo zinaweza kuwa kichocheo cha magonjwa ya ngozi.
Shirika hilo lilitoa mwezi mmoja tangu Juni 12, mwaka huu kuhakikisha nguo hizo zinaondolewa sokoni.
“Shirika limebaini kuwa nguo hizo licha ya kuwahi kupigwa marufuku mara kadhaa, zinaendelea kuwa katika masoko mbalimbali nchini na kwenye maduka tofauti ya mitaa, hivyo kufanya biashara hiyo ionekane kama imeruhusiwa ilhali si kweli,” lilieleza tangazo la TBS lililotolewa Juni.
Akizungumzia msako huo, Ofisa Uhusiano wa TBS Roida Andusamile, alisema mwezi mmoja waliotoa umeshapita lakini kinachoendelea sasa ni mchakato wa kazi hiyo kuanza.
Alisema msako huo utashirikiha askari mgambo na wataanza Dar es Salaam.
“Kinachoendelea sasa ni mawasiliano na manispaa zote tatu. Unajua tutatumia mgambo, sasa lazima uwaandalie utaratibu wa malipo ndiyo maana tumechelewa kuianza kazi hiyo lakini tunatarajia wiki ijayo,” alisema.
Kwa mujibu wa Andusamile, msako huo utakuwa mkali na kuwataka wafanyabiashara hao kuziondoa kwa hiari nguo hizo sokoni.
Awali Chama cha Wafanyabiashara wa Mitumba Mchikichini (MIMCO) waliiomba serikali kuwaongezea muda wa kuuza nguo zao ili kuepuka hasara.
Walilalamika kuwa muda uliotolewa na TBS ni mdogo kwani walikuwa wamekwisha agiza mzigo mkubwa ambao mitaji yao inatokana na mikopo waliyoipata kwenye benki na taasisi nyingine za fedha.
Baadhi ya nguo za ndani za mitumba zilizopigwa marufuku ni pamoja na chupi, sidiria, fulana, nguo za kulalia na soksi.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment