Ni wazi kwamba vita vya kupambana na dawa za kulevya si ndogo, kwani kwa namna inavyoonekana ni kwamba wenye kujihusisha na biashara hiyo, licha ya baadhi kudaiwa kushirikiana na wafanyakazi wasio waaminifu katika vyombo vya ulinzi, wanabuni mbinu tofauti kukwepa mkono wa sheria.
Tatizo la dawa za kulevya ni la dunia nzima, sio Tanzania au Afrika tu, kuna raia wengi wa kigeni wamenaswa nchini Colombia mwaka huu wakiwa na dawa za kulevya.
Katika tukio la jana, raia wa Canada, Tabitha Leah Ritchie (28) amekamatwa nchini Colombia baada ya kujaribu kupanda ndege kurejea Canada akiwa na tumbo bandia la ujauzito alimokuwa ameficha dawa ya kulevya aina ya Cocaine.
Leah aliyekuwa anajifanya mtalii akirejea Toronto, alihojiwa na polisi katika uwanja wa ndege wa Bogota. Polisi alimshuku na kumuuliza alikuwa amesalia na miezi mingapi kujifungua.
Alijibu kwa ukali mno , hali iliyomfanya ofisa mmoja wa polisi kumtilia shaka zaidi na kuamua kumfanyia ukaguzi zaidi.
Ofisa huyo aligusa tumbo na kuhisi lilikuwa baridi mno na Ngumu sana, ndipo wakaamua kumkagua zaidi.
Walimkuta na dawa za kulevya zilizokuwa zimefungwa ndani ya tumbo hilo bandia ambalo mwanamke huyo alikuwa amelivaa kwa kufunga tumboni.
Inasemekana alisema ana miezi saba ya ujauzito lakini baada ya polisi kumkagua walimpata na Cocaine kilo mbili iliyokuwa ndani ya vipochi viwili
Leah atashtakiwa na huenda akafungwa jela kwa miaka mitano au minane.
Mwaka huu pekee karibu watu 150 wamekamatwa na dawa za kulevya katika uwanja wa ndege wa Bogota.
Karibu theluthi moja ya waliokamatwa walikuwa raia wa kigeni, kwa mujibu wa maofisa wakuu nchini Colombia.
Wakati hayo yakiendelea nje, hapa nchini inabainika kwamba kushamiri kwa biashara ya dawa za kulevya kumeleta utamaduni mpya katika baadhi ya vijiwe vya vijana jijini Dar es Salaam.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment