Saturday, 7 September 2013

TAZARA RUDINI KAZINI JUMATATU-MWAKYEMBE


Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe.
Serikali imewaagiza wafanyakazi wote wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara), walioko kwenye mgomo kurejea kazini Jumatatu ijayo.

Agizo hilo lilitolewa na Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, wakati akitoa hoja za serikali bungeni mjini hapa jana.

Kadhalika alisema serikali ya Zambia imetoa Dola milioni tano sawa na Sh. bilioni nane kwa menejimenti ya Tazara wakati Tanzania nayo  imetoa Sh bilioni mbili kama fedha za dharura kwa mamlaka hiyo.

Dk. Mwakyembe alisema hatua ya kuwaagiza wafanyakazi hao wa Tazara kurejea kazini, inatokana na serikali kuwalipa mshahara wao wa Mei, mwaka huu huku mishahara mingine ya Juni, Julai na Agosti, ikiwa tayari imepelekwa benki na inatarajiwa kulipwa ifikapo Jumatatu ijayo baada ya taratibu za kibenki kukamilika.
  
Alisema fedha zilizotolewa na Tanzania pamoja na Zambia na dola milioni 3.17 za Marekani ambazo Tazara inadai kutoka kwa wateja wake mbalimbali, zinatosha kurejesha hali ya kawaida katika mamlaka hiyo.

“Hivyo basi, serikali inaiagiza menejimenti ya Tazara kudai madeni yote  kutoka kwa wadaiwa wake haraka iwezekanavyo ili ziingie mara moja kwenye matumizi ya mamlaka," alisisitiza Waziri Dk. Mwakyembe.

Alisema mgomo huo wa watumishi wa Tazara uliodumu kwa takribani wiki mbili sasa kuanzia mwezi uliopita umeisababishia mamlaka hiyo hasara ya zaidi ya dola milioni 1.4 hadi kufikia Septemba 2, mwaka huu.

Dk. Mwakyembe alifafanua kuwa mgomo huo ulisababisha treni 13 zenye mabehewa 252 yenye mizigo ya tani 10,080 kukwama njiani.

Alisema mizigo iliyomo kwenye mabehewa hayo ni tani 3,600 za shaba, tani 630 za manganizi, tani 3,015 za mbolea, tani 500 za saruji,  tani 1,170 za mafuta na tani 1,665 za bidhaa mchanganyiko.

Kadhalika, Waziri Mwakyembe alisema mbali ya Tazara kupata hasara hiyo, pia wakazi 46,000 wa jijini Dar es Salaam, wameathirika vibaya na mgomo huo kwa kukosa huduma ya mjini waliyoizoea.

Vile vile, alisema abiria 24,000 wenye tiketi wakiwamo watalii ambao walikosa usafiri wa treni na Tazara ikalazimika kuwarejeshea nauli zao .

Kwa msingi huo, Dk. Mwakyembe aliwataka wafanyakazi hao wa Tazara kurejea kazini Jumatatu asubuhi na kuchapa kazi kwa bidii ili kufikidia hasara hiyo iliyopatikana.

Wafanyakazi hao waliingia katika mgomo unaoingia wiki ya pili wakidai mishahara ya miezi minne, mameneja saba kufukuzwa kazi, kurekebishwa kwa sheria ya Tazara na Mwendesha garimoshi Mkuu wa mkoa wa Tanzania, Theresia Mahagatila kurudishwa kazini bila masharti yoyote.

Madai mengine ni kutaka kumwona Waziri Mkuu, Mizengo Pinda pamoja na kulindwa kwa haki za wafanyakazi wa shirika hilo. Mwenyekiti wa Taifa a Chama cha Wafanyakazi wa Reli(TRAWU, Mussa Kalala alisema kitu muhimu wanachohitaji ni matatizo yao  kupatiwa ufumbuzi wa kudumu na siyo wa muda.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...