Thursday 12 September 2013

UFISADI HALMASHAURI YA JIJI DAR ES SALAAM



Dar es Salaam: Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ilikiuka taratibu za utoaji wa zabuni ya kubomoa jengo lililokuwa ndani ya Kituo Kikuu cha Mabasi yaendayo mikoani kilichopo Ubungo (UBT), ambalo lilianguka mwanzoni mwa mwaka huu na kusababisha madhara kwa watu na mali. Januari 21 mwaka huu, watu wanne walijeruhiwa baada ya magari yao waliyokuwa wameyaegesha katika eneo la UBT kuangukiwa na ukuta, huku magari 24 na bajaji nne zikiharibika vibaya.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa Kampuni ya Makalla Contractors Ltd ndiyo iliyofanya kazi ya ubomoaji huo, lakini hakukuwa na mkataba wa kazi hiyo baina yake na Jiji la Dar es Salaam.
Uchunguzi zaidi unaonyesha kuwa, licha ya kutokuwa na mkataba, Makalla Contractors Co. Ltd wamepeleka kwa uongozi wa jiji hilo madai ya Sh59, 615, 252 wakitaka walipwe kutokana na kazi hiyo.
“Makubaliano yalifanyika kwa mdomo na kazi ikaanza, hakukuwa na uitishwaji wa zabuni wala kufanyika taratibu zozote za kisheria, walipeana kazi hiyo kirafiki na baada ya jengo kubomoka ndipo walianza kuhaha jinsi ya kuwezesha kulipa fedha hizo,” kilisema chanzo chetu.
Katika moja ya nyaraka za kampuni hiyo kwenda Halmashauri ya Jiji, Kampuni hiyo ya Makalla inasema ilipewa kazi hiyo kutokana na gharama zake kuwa za chini na kwamba iliombwa kuanza kuitekeleza haraka kutokana na udharura wake kwa ahadi kuwa taratibu nyingine za kupewa LPO na mkataba zingefuata. Hata hivyo, taratibu za zabuni zinataka kazi itangazwe na hata kama kungekuwa na dharura ilipaswa kufuata utaratibu wa ‘single sourcing’ ambao ungewezesha kuchagua kampuni ya kutekeleza jukumu bila kuchelewa. Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk Didas Masaburi ambaye ndiye mwenye dhamana ya kusaini mikataba kwa niaba ya jiji hilo alisema: “Sijawahi kusaini mkataba unaohusu kampuni hiyo unayoitaja (Makalla) na wala sijawahi kusaini mkataba kuhusu ubomoaji wa pale Ubungo.” Alipobanwa akitakiwa aeleze sababu za ubomoaji kufanywa bila yeye kuhusishwa alijibu: “Waulize watendaji wa Jiji, muulize mkurugenzi maana huo ni wajibu wa watendaji na siyo wajibu wa Meya, nilichokwambia ni kwamba mimi sijasaini mkataba wowote kuhusu suala hilo.”
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Wilson Kabwe alipoulizwa alisema hawezi kutoa taarifa kuhusu suala hilo kwenye vyombo vya habari.
“Wewe hizo taarifa umezipata wapi?... Mimi siwezi kukwambia mkandarasi gani aliyehusika, sitoi taarifa hizo kwenye vyombo vya habari… unazitaka za nini? Wananchi ndio wamekutuma uwatafutie taarifa? Wao wanatakiwa wasubiri huduma ikamilike, lakini siyo kumjua mkandarasi, kalipwa au hakulipwa,” alisema Kabwe.
Malipo kwa Mkandarasi
Wakati Kabwe akihoji maswali lukuki, habari zaidi zinasema ofisi yake imekuwa katika harakati za kuwezesha Kampuni ya Makalla kulipwa, na kwamba kinachokwamisha malipo hayo ni kutokuwapo kwa mkataba wa kazi. Fedha za ubomoaji kiasi cha Sh63 milioni zilitolewa na Ofisi ya Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) na kuhamishiwa kwenye akaunti za Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, lakini imebainika kuwa kumekuwapo na harakati za fedha hizo kurejeshwa DART.
“Ofisi ya mkurugenzi inaendelea na mchakato wa kurejesha fedha hizo DART ili Kampuni ya Makalla ikalipwe huko maana ni ngumu malipo kufanyika hapa kwetu kwa sababu hakuna documents (nyaraka) za mkataba wa kazi, huwezi kulipa, sasa huko DART nao sijui watafanyaje,”kilidokeza chanzo chetu katika ofisi za Jiji. Hata hivyo, Ofisa Mwandamizi wa DART, Jack Meena alisema suala hilo linawahusu Wakala wa Barabara Nchini (Tanroads) na Halmashauri ya Jiji ambao ndiyo wamiliki wa kituo hicho.
“Sisi kazi yetu ni kuhakikisha eneo la mradi linakuwa tayari kwa ajili ya ujenzi. Kwa hiyo tulifanya tathmini na kulipa fidia na kumwachia mkandarasi,” alisema Meena.
Msimamizi wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka katika Tanroads, Barakaeli Mmari alisema suala hilo linashughulikiwa na Halmashauri ya Jiji, hivyo waulizwe wenyewe.
CHANZO: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...