Chacha Makenge akitoka kwenye handaki lake. Picha na Florence Majani.
Tunaposikia handaki, fikra zinatupeleka moja kwa moja kwenye vita kwani aghalabu, mahandaki hutumiwa na watu kujificha wakati wa vita.
Hata hivyo, ugumu wa maisha umesababisha baadhi ya watu kuyageuza mahandaki kama makazi ya kuishi.
Ni katika Barabara ya Sam Nujoma, natoka Ubungo kuelekea Mwenge, nashuka mita chache kabla ya kufika Mlimani City, naingia katika pori lililo nyuma ya Ukumbi wa Mlimani City.
Hakuna njia maalumu ya kuingia katika pori hili. Hatua kwa hatua napita katikati ya vichaka na nyasi ndefu, hatimaye nafika katika eneo tofauti. Ni kama bustani iliyotengenezwa na mbunifu wa hali ya juu.
Miti imefyekwa kwa utalaamu wa hali ya juu, baadhi ya vichaka vimepunguzwa kwa umahiri na kutengeneza umbile zuri mfano wa maua yaliyotengenezwa. Lakini, mwisho kabisa wa mandhari hii kuna mianzi imelazwa chini na pembeni kuna shimo.
Shimo hilo ndilo handaki analoishi Chacha Makenge, kijana mwenye umri wa miaka 36, mzaliwa wa Mugumu Wilaya Serengeti Mkoa wa Mara kwa muda wa miaka minne sasa.
Hata hivyo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Makenya Maboko anasema kuwa hana taarifa zozote kuhusu Makenge kuishi katika eneo hilo.
“Sina taarifa, wewe ni mtu wa kwanza unanipa habari hizi, ngoja nilifanyie kazi,” anasema Profesa Maboko.
Jirani na handaki hilo namkuta Makenge akifyeka majani kwenye bustani yake. Ananikaribisha na tunaingia katika handaki hilo. Ni shimo refu, kwani tunatakiwa kushuka ngazi tatu kubwa kwenda chini. Ndani kuna kitanda cha kamba na miti kilichofunikwa kwa magunia na shuka kadhaa.
Ukuta ambao ni udongo, umechongwa mithili ya meza ndogo ambayo Makenge ameweka kioo, kitana, boksi lenye dawa mbalimbali na mswaki.
Upande wa kulia wa handaki hili kuna misumari iliyopigiliwa katika ukuta huo ambapo Makenge ametundika makoti na suruali, ambazo bila shaka ni zake.
Upande wa kushoto, Makenge kwa kutumia ukuta huo huo, ametengeneza meza nyingine ambayo imewekwa chupa za plasitiki za maji ya kunywa.
Makenge anasimulia kuwa, alifika jijini Dar es Salaam mwaka 1996, kutafuta maisha akitokea kijijini kwao Kisangula mkoani Mara. Anabainisha kuwa alifikia Tabata, Segerea kwa babu yake mzaa mama, aliyemtaja kwa jina la Mzee Mwita Mahende.
Kwa kuwa alikuwa ni kijana asiyekuwa na ujuzi wowote, alianza kufanya biashara ya kuuza mayai ya kuku wa kisasa na kienyeji kwa kuyatembeza barabarani.
“Nilipoona biashara nzuri, nilitafuta kibanda na nikaanza kuuza mayai yangu maeneo ya Mwenge,” anasema Makenge.
Lakini Manispaa ya Kinondoni walibomoa banda lake na baada ya hapo aliamua kubadilisha biashara na kuanza kuuza vyuma chakavu.
“Hata hivyo, niliacha kuuza vyuma chakavu baada ya kusikia taarifa kuwa kuna mtoto ameokota bomu dogo la mkononi akidhani ni chuma chakavu,” anasema.
Baada ya kuacha biashara hiyo, aliamua kujiunga na Chuo cha Sanaa Bagamoyo ambako alijifunza sanaa za uchongaji.
Aliporudi kutoka Bagamoyo, aliamua kutumia ujuzi huo pamoja na kipaji chake kuanzisha kitu kitakachovutia na kumwingizia kipato. Hata hivyo, hakuwa na eneo la kufanyia kazi zake na alimwomba rafiki yake (jina tunalo), eneo ili atengeneze bustani na kuuza zana zake anazochonga.
“Nilitengeneza lile eneo kwa kudizaini bustani kubwa yenye viti vya miti asilia, maua mazuri na majani ya ukoka. Likawa eneo zuri mno kiasi kwamba nikaanza kutoza watu fedha ili wafanyie sherehe au mapumziko,” anasema.
Hata hivyo, kabla hajaendeleza vizuri eneo hilo, rafiki yake alimwambia aondoke kwani analitaka eneo lake. Rafiki yake huyo hakuja hivi hivi, alikuja na polisi. “Siku moja usiku nikiwa nimelala walikuja watu watatu wakaanza kuniamrisha nipige magoti, wakanipiga na mimi nikaanza kujihami, lakini wao walikimbilia polisi na nikaja kukamatwa,” anasema.
Alikamatwa na polisi na kushtakiwa kwa kujeruhi jambo ambalo Makenge anakana akiamini yeye siyo mkosaji na kuamua kufanya mgomo wa kula akiwa mahabusu.
“Nikiwa magereza niliamua nifunge kula, lakini polisi walinipeleka hospitali na baadaye eti wakagundua kuwa nina matatizo ya akili,” anasimulia akishangaa.
Wodi ya wagonjwa akili
Makenge anasema hakuelewa kwa nini aliambiwa ana ugonjwa wa akili, kwani hajawahi kuwa na historia hiyo tangu kuzaliwa kwake, hata kusikia.
Alipelekwa wodi ya wagonjwa wa akili katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili(MNH), ambako alianzishiwa matibabu anayosema hakuelewa ni ya nini. “Nilikuwa pale na nilitibiwa na Dk Sylvia Kaaya. Walikuwa wananipa dawa, lakini sikuwa nikizimeza na nilizitupa kwa sababu sielewi napewa dawa kwa ugonjwa upi,” anasema.
Anasema kuwa akiwa wodini hapo alikataa kula chakula akihofia kuwekewa dawa ndani yake jambo ambalo lilisababisha wale chakula pamoja na daktari wake. Baada ya miezi miwili, alitolewa na kupandishwa tena mahakamani ambako alihukumiwa kifungo cha miezi tisa kwa kosa lilelile la kujeruhi. Kwa bahati nzuri, Makenge alipata msamaha wa Rais baada ya kukaa jela kwa muda wa miezi minne.
Alipotoka jela maisha hayakuwa mepesi tena na alijaribu kazi ya kusafisha viatu (shoe shine) akilala sehemu yoyote yenye kibaraza, lakini haikumsaidia na baadaye aliamua kuzunguka katika mitaa ya jiji huku na huko akitafuta riziki.
Kwa kuwa alipenda kukaa maeneo ya Ubungo karibu na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, aliligundua eneo hili ambalo lipo nyuma ya chuo hicho, akaamua kuanzisha makazi.
“Niliona ni sehemu isiyo na kelele. Imejificha na ina vichaka. Nikaamua nisijenge banda, kwani linaweza kuvunjwa au kuleta mgogoro kwa sababu siyo eneo langu,” anasema.
Aliamua kuchimba handaki ambalo aliamini lisingeweza kuathiri mazingira. Hata hivyo, hakuishia kuchimba handaki tu, bali aliyapamba mandhari ya eneo hilo kwa kutengeneza bustani ya maua na sehemu za kupumzika.
Anasema kuwa awali baada ya kuanza kuishi katika handaki hilo, Kitengo cha Usalama Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kilifika na kumhoji kwa kina, lakini baadaye waliona anatunza mazingira na wakamwacha.
“Nimeishi hapa kwa muda wa miaka minne tangu Januari 2010. Na ninayafurahia mazingira haya ili mradi sivunji sheria za nchi,” anasema Makenge.
Makenge anasema kuwa wanafunzi wengi wa UDSM wanamfahamu na hufika kumtembelea au yeye kuwatembelea.
Hata hivyo, Makamu wa Rais wa Serikali ya Wanafunzi ya Chuo hicho(Daruso), Emmy Mwamgiga aliyemaliza muda wake wa uongozi mwaka huu, anasema hajawahi kusikia taarifa za mtu huyo.
“Ni jambo linalonishangaza sana, nimesoma katika kipindi chote hicho, wala sijawahi kusikia kama kuna mtu anaishi kwenye handaki karibu kabisa na chuo chetu,” anasema. Mwamgiga.
Kipato chake
Makenge ni mtu mwenye kipaji, licha ya kuchonga zana mbalimbali kama fimbo, vigoda, chanuo na vibao vya urembo, anaweza pia kutengeneza bustani kwa ustadi mkubwa na vitu hivyo, ndivyo vinavyompa mkate wake wa kila siku.
Katika makazi yake haya, Makenge anaishi kama watu wengine; anapika, anafua, anaoga na anasoma magazeti na vitabu mbalimbali vilivyomo katika handaki lake. Pia anasema, duka lake kubwa ni Supermarket ya Shoprite iliyopo Mlimani City.
Siku niliyokwenda kumtembelea, alikuwa akiwasha moto wa kuni na kubandika maharage.
Jambo la kushangaza kuhusu Makenge ni kuwa licha ya elimu yake ya darasa la saba, ana ufahamu mkubwa wa mambo ikiwamo mchakato wa Katiba Mpya, uongozi, siasa, masuala ya afya na ukusanyaji kodi.
Itaendelea wiki ijayo
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment