Tuesday, 24 December 2013

Usafiri wa Krismasi majanga UBT


Abiria katika kituo Kikuu cha mabasi yaendayo mikoani,ambapo wamelamikia  ongezeko kubwa la nauli ambazo sasa zimefikia Sh70,000 kutoka Sh23,000 kwa mabasi ya kwenda katika Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Mbeya na Iringa. 

Dar es Salaam/Moshi. Mamia ya abiria, wamekwama kusafiri katika Kituo Kikuu cha Mabasi yaendayo mikoani na nchi jirani cha Ubungo  jijini  Dar es Salaam kutokana na upungufu wa mabasi.
Abiria hao pia wamelamikia  ongezeko kubwa la nauli ambazo sasa zimefikia Sh70,000 kutoka Sh23,000 kwa mabasi ya kwenda katika Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Mbeya na Iringa.
Imeelezwa kuwa pamoja na maofisa wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) kuweka kambi kituoni hapo, lakini wameshindwa kukabiliana na hali hiyo.
Ofisa Leseni wa Sumatra, Sebasitia Lohay alisema ongezeko la abiria kipindi hiki cha sikukuu ni la kawaida na kwamba hakuna tatizo la usafiri.

“Hakuna tatizo la usafiri na ni kawaida kuwa na idadi kubwa ya abiria katika kipindi hiki…tunaendelea kukagua nauli na kuwatoza faini watakaobainika kupandisha nauli,” alisema Lohay jana asubuhi.
Mwananchi iliyokuwepo kituoni hapo mapema asubuhi, ilishuhudia abiria wengi wakiwa hawafahamu cha kufanya baada ya kukosa usafiri.
Pia, Mwananchi ilishuhudia mabasi aina ya Coaster yakiwa yamejaa abiria wanaokwenda Mikoa ya Kilimanjaro na Arusha.
Wakizungumza na waandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti, abiria hao walikiri kuwa hali ya usafiri katika kituo hicho ni mbaya na kwamba upungufu wa mabasi umesababisha ongezeko la nauli hadi kufikia Sh70,000.
Tatizo la upungufu wa mabasi na kuongezeka kwa nauli za mabasi katika Kituo cha Mabasi cha Ubung0, linajitokeza kila mwaka na kusababisha malalamiko kutoka wananchi wanaotaka kusafiri ili kwenda makwao kusherehekea sikukuu.
Baadaye, tatizo hilo linawakumba wananchi hao katika mikoa yanayokwenda na mara kadhaa wanalazimika kusafiri kwa malori kurejea jijini Dar es Salaam.
Mkesha wa Krismasi


Mkesha wa Sikukuu ya Krismasi utafanyika leo kitaifa kwenye Kanisa Kuu la AIC (Africa Inland Church) mkoani  Geita.
Katibu Mkuu wa CCT, Dk Leonard Mtaita, alisema jana mkesha huo,  utafuatiwa na ibada itakayofanyika kesho kwenye Kanisa la Katoliki Dayosisi ya Geita.
“Ni utaratibu wetu kuzunguka katika mikoa, mwaka jana ilikuwa Moshi na safari hii tuko Geita,” alisema.
Moshi yafurika
Mji wa Moshi na vitongoji vyake umeanza kuzizima kwa ongezeko kubwa la wageni na magari huku baadhi ya barabara zikiwa na msongamano mkubwa wa magari.
Wingi wa magari na wageni katika mji huo, unatokana na utamaduni uliozoeleka wa wakazi wa Mkoa wa Kilimanjaro wa kurejea mkoani humo kila mwisho wa mwaka, ili  kusherehekea sikukuu za mwisho wa mwaka na mwaka mpya.
Msongamano mkubwa upo katika Barabara ya Nyerere, Sokoni na zile za katikati ya mji kwenye maeneo ya biashara ambako hata maeneo ya maegesho sasa yamekuwa shida.
Jeshi la Polisi limelazimika kuweka askari wa usalama barabarani katika baadhi ya barabara ili kuongoza magari kutokana na misururu mirefu ya magari.
Katika Kituo Kikuu cha mabasi cha mjini Moshi, abiria wengi wamekuwa wakiwasili kutoka nje ya mkoa huo.
Hata hivyo  idadi ya wale wanaosafiri kutoka Kilimanjaro kwenda nje ya mkoa huo ni ndogo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz, aliliambia gazeti hili jana kuwa polisi wamejipanga kikamilifu kukabiliana na ongezeko la watu na magari .
Miti yadoda
Wafanyabiashara wa miti na mapambo maalumu yanayotumika wakati wa Sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya, wamelalamikia kukosa wateja hali inayosababisha bidhaa zao kudorora.
Mwananchi lilishuhudia  baadhi ya wafanyabiashara  hao maeneo ya Mwenge, Manzese na Sinza, wakiwa wamezungukwa na miti pamoja na mapambo wakisubiri wateja bila mafanikio.
Miti hiyo huuzwa kati ya Sh 15,000 na Sh 12,000 wakati  bei za mapambo mengine zikitofautiana kutokana na aina ya maua ya mapambo.
Etikody Chogo, mmoja wa wafanyabiashara katika Stendi ya Mwenge alisema gharama za miti na mapambo ya Krismasi zimekuwa za juu mno ikilinganishwa na mwaka jana.
“Watu hawanunui sana kama ilivyokuwa mwaka jana biashara haijachangamka kabisa nadhani ni kutokana na hali ya uchumi,” alisema Chogo.
*Imeandaliwa na Daniel Mjema, Aidan Mhando na Elizabeth Edward wa Mwananchi

No comments:

Post a Comment

PALM TREES ARE BEAUTIFUL

Minazi huleta mandhari nzuri ya kuvutia, haijalishi ni sehemu gani imemea. Palm trees are always beautiful, it doesn´t matter where they are...