Hatutakiwi kuomboleza juu ya kumpoteza Nelson Rolilahla Mandela maarufu kama "Madiba" bali tusherehekee kwa kuwepo kwake na mafundisho ambayo ametuachia.
Mandela ameifundisha dunia namna ya kusamehe na usawa,kujali utu wa mtu n.k.Madiba hakuwa na tamaa ya kujilimbikizia mali kama walivyo viongozi weni. Ingawa alikaa jela miaka 27 hakutaka kulipa kisasi. Waliomfunga na kuwabagua watu weusi yeye alisema "hawa ni rafiki zetu". Ni kiongozi gani wa Afrika wa sasa anaweza kukubali haya?Hakika viongozi wetu wa Afrika wana mengi sana ya kujifunza kutoka kwa Madiba.
Mandela ametumia sehemu kubwa ya maisha yake gerezani. Ni baba na mume ambaye aliwekwa mbali na familia yake.Hakuweza kuwakuza watoto wake kama wafanyavyo baba wengine. Hakuweza kuwa karibu na mkewe kama wafanyavyo waume wengine.Hii ilitokana na utawala dhalimu wa kibaguzi wa Apartheid.
Mandela amehamasisha viongozi wengi wakubwa na maarufu duniani kati yao akiwemo rais wa sasa wa Marekani,Barack Obama ambaye alikiri hili kwa maneno yake mwenyewe.
HISTORIA YA MADIBA
1918: 18 Julai Rolihlahla Mandela alizaliwa
1924: Rolihlahla Mandela alianza shule na mwalimu wake akampa jina la "Nelson"
1942: Alianza kuhudhuria mikutano ya chama cha ANC.
1944: Alikuwa ni mmoja wa waanzilishi wa ANC Youth League(ANCYL)
1941: Alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa ANCYL.
1952: Alikamatwa na kuhukumiwa adhabu ya kazi ngumu kwa muda wa miezi 9.Mwaka huu vilevile alianzisha ofisi ya kwanza kutoa ushauri wa kisheria(Law firm) ikimilikiwa na watu weusi akishirikiana na Oliver Tambo.
1958: Aliachana na mkewe wa kwanza na kuoana na Winnie Madikizela.
1960: Mandela pamoja na watu wengine walikamatwa.
8 Aprili ANC apigwa marufuku.
1962: 11 Januari Mandela aondoka Afrika ya kusini kwaajili ya mafunzo ya kijeshi.
5 Augusti akamtwa na kuhukumiwa kifungo cha miaka mitano kwa kuondoka nchini bila ruhusa.
1963: Mandela afikishwa kisiwani Robben.
1964: Ahukumiwa kifungo cha maisha.
1984: Wimbo "Free Nelson Mandela" wawa kibao maarufu duniani.
1990: 2 Februari: ANC yaanza shughuli zake tena.
11 Februari Nelson Mandela aachiwa huru!
1993: Nelson Mandela atunukiwa tuzo ya heshima ya amani ya Nobel.
Nelson Mandela akiwa na mshindi mwenzie wa tuzo ya amani ya Nobel Fredrick De Klerk
1994: 9 Mei Nelson Mandela aapishwa kama rais mweusi wa kwanza wa Afrika ya kusini.
2013: Mandela alikimbizwa hospitalini mara kadhaa kutokana na kuzorota kwa afya yake kufuatia matatizo ya mapafu kulikosababishwa na ugonjwa wa kifua kikuu aliougua akiwa gerezani.
5 Desemba Nelson Mandela afariki.
Kufuatia kifo cha Mandela bendere za nchi mbalimbali zinapepea nusu mlingoti ikiwemo Tanzania, Marekani ,Uingereza na Afrika ya kusini yenyewe. Mungu ailaze roho ya Nelson Mandela mahali pema peponi,amen.
Imetayarishwa na Anna Nindi kwa msaada wa vyombo vya habari mbalimbali.
No comments:
Post a Comment