“Kwa kuzingatia kuwa dawa za kulevya ni kosa la jinai na athari zake ni kubwa ikiwa ni pamoja na kuzorotesha nguvukazi za vijana, ni vyema raia wakiona mtu wanayemshuku kuhusika na biashara hiyo watoe taarifa haraka na sisi tutachukua hatua haraka,’’Kamanda Shilogile.PICHA|MAKTABA
Morogoro. Mwili wa aliyekuwa mfanyabiashara wa Kariakoo, Dar es Salaam, Khalid Kitara (47) uliokutwa na dawa za kulevya zinazodhaniwa kuwa ni heroini, umekabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya utaratibu wa mazishi.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya kukamilika kwa uchunguzi wa madaktari wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile aliwaambia waandishi wa habari mjini hapa jana kwamba baada ya kufanyika kwa uchunguzi huo wameamua kukabidhi mwili huo huku wakiendelea na upelelezi kubaini mtandao unaohusika na tukio hilo.
Alisema jeshi hilo bado linaendelea kuwashikilia watuhumiwa watatu, ambao ni madereva wawili waliokuwa wakipokezana kuendesha gari hilo ambao aliwataja kuwa ni TeddySichilima (27), mkazi wa Tunduma Mbeya, Lucas Atubonekisye (32), mkazi wa Mtaa wa Songea, Tunduma na aliyekutwa na mwili wa Marehemu, Jumbe Mbano (36), mfanyabiashara na mkazi wa Kariakoo. Alisema watu hao watafikishwa mahakamani wakati wowote baada ya uchunguzi kukamilika.
Alitoa wito kwa jamii kuendelea kuwafichua wahalifu ili sheria ichukue mkondo wake huku akisisitiza azma ya polisi kupambana kuhakikisha linatokomeza biashara ya dawa ya kulevya ambazo kwa sasa uuzaji wa dawa hizo umeonekana kuzagaa nchini.
CHANZO: MWANANCHI
No comments:
Post a Comment