Foleni jijini Dar es salaam
Kuna kila dalili kuwa jinamizi la foleni litaendelea kuwatesa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kwa muda mrefu zaidi kutokana na kasi ndogo ya utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa barabara za pembezoni (ring roads) na usanifu wa barabara za juu (flyig overs) ambayo kwa ujumla inahitaji walau Sh. bilioni 170.
Kero hiyo itapungua kwa kiasi kikubwa ikiwa fedha hizo zitapatikana ili kutekeleza miradi mbalimbali iliyopewa kipaumbele katika kukabili tatizo hilo.
Uchunguzi uliofanywa na NIPASHE hadi kufikia mwisho wa wiki iliyopita, umebaini kuwa ujenzi wa barabara za pembezoni unaendelea kwa kasi ya kinyonga huku ujenzi wa barabara za juu kwenye makutano ya barabara kuu ukiwa ndiyo kwanza uko katika hatua ya usanifu.
Aidha, jumla ya Sh. bilioni 171.2, ambazo ni sawa na asilimia 14 ya bajeti yote ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka huu wa fedha wa 2013/2014, ni sehemu tu ya mikakati iliyopewa kipaumbele katika utekelezaji ili kupunguza foleni jijini Dar es Salaam ikihusisha usanifu wa barabara za juu (Sh. bilioni 100), ujenzi barabara ya Kigogo – Jangwani (Sh. bilioni 7.6), fidia kwa majengo ya kandoni mwa barabara ya Kigogo-Jangwani (Sh. bilioni 15.8) na kipande cha kilomita tatu cha barabara ya Kimara Korogwe- Kilungule kinachogharimu Sh. bilioni 3.5.
Fedha nyingine ni Sh. bilioni 13 kwa ajili ya kilomita saba za Mbezi Mwisho-Goba, Sh. bilioni 16 za Tangi Bovu-Goba, Baruti-Msewe (Sh. bilioni 4.6) na Kigogo- Tabata Dampo (Sh. bilioni 5.7).
HALI ILIVYO
Hakika, katika jiji la Dar es Salaam kunahitaji uvumilivu wa hali ya juu, hasa kuhusiana na usafiri wa kutoka sehemu moja kwenda nyingine nyakati za asubuhi na jioni.
Kiukweli, unaweza kujikuta usingizi wako ukiathiriwa na jinamizi la foleni. Unalala ukiwaza foleni itakavyokutesa asubuhi wakati ukienda au kurejea kutoka katikati ya jiji kusaka mkate wa kila siku.
Tatizo huwa kubwa zaidi kwa wakazi wa pembezoni mwa jiji. Kwa mfano, wanaoishi maeneo ya nje ya katikati ya jiji kama Tabata Segerea, Kinyerezi, Kibamba, Bunju na Kivule, hali huwa mbaya zaidi. Ni zaidi ya kero. Ni adhabu kubwa!
Mbaya zaidi, wakati mwingine adha hii huwa haichagui nyakati. Ni kawaida pia kukuta foleni kubwa ya magari mchana na hata usiku wa hadi saa 5:00.
Matokeo yake, siyo jambo geni kujikuta ukitumia jumla ya saa tatu hadi sita kwa safari ya kwenda maeneo ya katikati ya mji na kurudi.
Wananchi wa kawaida ambao wengi hutegemea usafiri wa daladala hujikuta wakikumbana na adha nyingine ya kupata usafiri huo kwani magari huwa haba kwa vile hutumia muda mwingi yakiwa yamesimama tu barabarani kutokana na foleni. Na gari linapofika kituoni, ni wenye nguvu tu ndiyo hujihakikishia siti huku wengine wakihaha walau kupata upenyo wa kuingia garini.
Wagonjwa, wajawazito, watoto na wazee huwa ni waathirika wakubwa kwani huwa hawawezi kupigania daladala hizi.
Wakati mwingine, unalazimika kutumia gharama maradufu kufika maeneo ya kati ya mji kwani mahali pa nauli ya Sh.400, unaweza kutumia Sh. 2,000 kwa kuwa madereva na makondakta wamegeuza mtaji kwa kupakiza abiria vituo vya mwanzo na kwenda nao hadi mwisho na kugeuka nao hata kama gari limejaa.
Mbali na kuwa kero kwa watumiaji wa barabara, foleni za magari pia husababisha athari za uchafuzi wa mazingira kwani magari hutumia muda mwingi barabarani na kutoa moshi (ulio na gesi ukaa) kwa wingi.
Zipo pia athari kubwa za kiuchumi kutokana na foleni ndefu za mara kwa mara katika barabara za jiji la Dar es Salaam kama Morogoro, New Bagamoyo, Kilwa, Kawawa, Mandela na Nyerere.
Kwa mfano, utafiti uliofanywa na kitengo cha takwimu cha Kampuni ya The Guardian Limited chini ya usimamizi wa Edward Ntwale, ulibaini kuwa msongamano wa magari katika jiji la Dar es Salaam unaipotezea serikali mapato ya Sh. bilioni 411 kila mwaka, huku wafanyakazi wanaotumia usafiri wa daladala wakipoteza saa mbili barabarani kila uchao.
Aidha, kati ya fedha hizo, Sh. bilioni 120.4 zinapotezwa na waajiri kila mwaka kwa kuwalipa wafanyakazi kwa saa ambazo hawafanyi kazi huku wamiliki wa daladala wakipoteza Sh. bilioni 265.6 na gharama za mafuta ya ziada kwa wamiliki wa magari zikiwa ni Sh. bilioni 25.6 kwa kipindi hicho.
Kulingana na utafiti huo, kiasi hicho cha fedha kinachopotea kwenye foleni ya magari kila mwaka kingeweza kugharimia ruzuku ya mbolea kwa mwaka wa fedha 2013/14 na chenji ikabaki, kwa kuwa serikali katika bajeti ya mwaka 2013/14 imetenga Sh. bilioni 349.2 pekee kwa ajili ya ruzuku ya mbolea.
Aidha, fedha hizo pia ni zaidi ya makisio ya serikali ya kukusanya Sh. bilioni 383.5 kutoka halmashauri kwa mwaka huu wa fedha.
Katika barabara ya Morogoro ambako hivi sasa kuna ujenzi wa barabara ya mabasi yaendayo kasi (Dart), hali ni mbaya kwa kupita kiasi. Kwa sasa hakuna nafuu kwa nyakati za asubuhi, mchana wala usiku. Muda wote huwa kuna foleni na kila dereva hujitahidi kuhakikisha kuwa anaingia kwenye barabara hizi finyu ili kuwahi anakotaka kwenda.
Inapotokea ajali, hata kama ni ndogo kiasi gani, mateso ya foleni huongezeka maradufu.
Kupunguza au kumaliza kabisa foleni jijini Dar es Salaam kunahitaji mipango thabiti na utekelezaji kivitendo wa kila kinachoelezwa.
Hata hivyo, kinachoonekana ni kuwa kasi ya kukabiliana na adha ya foleni jijini Dar es Salaam haiendani na ongezeko la magari barabarani. Na ofisi nyingi muhimu za serikali na binafsi zinaendelea kuelekezwa katika maeneo ya katikati ya jiji, hasa Posta, Upanga na maeneo ya jirani.
“Imekuwa ni kawaida kuamka saa 10:00 alfajiri na kurudi nyumbani kwangu saa 5:00 usiku. Foleni inanifanya siku zote kuwa mgeni kwa familia yangu. Nashindwa kuonana na wanangu kwa wakati, nikitoka wamelala, nikirudi wamelala,” ndivyo anavyoeleza Nassari Kitoi, mkazi wa Mbezi Madale, eneo lililopo katika Manispaa ya Kinondoni, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
Kitoi anasema kuwa kwa uzoefu wake, anajua kuwa siku za Jumanne hali ya foleni huwa ni mbaya zaidi kwani ni siku mojawapo ambayo magari yanayosafirishwa kwenda nje ya nchi kutoka katika Bandari ya Dar es Salaam huondoshwa kwa wingi zaidi.
Kitoi anasema kuwa ili aweze kufika kazini kwake saa 2:00 asubuhi, hulazimika kutoka nyumbani kwake saa 11:00 alfajiri kwani nyakati hizo huwa kuna nafuu kubwa.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment