Anuradha Sharma |
Ujumbe wa uongozi wa juu wa Shirika la Afya la Paras la nchini India linalomiliki hospitali za ngazi ya kimataifa, umewasili jijini Dar es Salaam jana, pamoja na mambo mengine umeanza mchakato wa kuwekeza katika sekta ya afya nchini.
Ujumbe huo ukiongozwa na Naibu Meneja wa hospitali hizo anayehusika na uhusiano wa kimataifa, Anuradha Sharma, ulipokelewa na Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Yono Auction Mart ambaye ni Mbunge wa zamani wa Njombe Magharibi, Yono Kevela.
Akizungumza baada ya kuwasili, Sharma alisema ujumbe huo umekuja kutokana na uongozi wa juu wa shirika hilo kuridhika na mazingira ya uwekezaji nchini ikiwa ni pamoja na uhakika wa uendeshaji wa serikali, sera madhubuti na hali ya amani na utulivu.
Alisema ni lengo la uongozi wa hospitali hizo ambazo zinashika nafasi ya juu katika utoaji wa huduma za afya nchini India zikiwa na matawi makubwa katika miji ya Haryana, Patna, New Delhi na Darbhanga , kuona kuwa hospitali hizo zinajengwa Afrika na hasa Tanzania, Nigeria na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
“Ni madhumuni yetu sasa kuona kuwa tunatoa huduma bora za afya kutoka katika pande zote za Dunia, lakini kwa kuangalia maeneo ambayo ni rafiki kwa uwekezaji Tanzania ikiwa ni moja ya mataifa tunayoyalenga,” alisema Sharma.
Alisema pamoja na mambo mengine ziara yao inalenga kuonana na sekta mbalimbali wakiwamo viongozi wa serikali na wa sekta binafsi kwa lengo la kuanza kwa mchakato wa kulifanya shirika hilo kuanza kuwekeza katika sekta ya afya hapa nchini.
Alisema Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo la Paras, Dk. Dharminder Nagar, ameridhishwa na jitihada zinazofanywa na Serikali ya Rais Jakaya Kikwete katika kuboresha sekta ya afya hatua ambayo imemfanya kukubali shirika hilo kuanza mchakato wa kuwekeza kwa kushirikiana na wawekezaji wazalendo.
Akizungumzia ziara hiyo, Yono alisema pamoja na mambo mengine ujumbe huo utaonana na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid na pia utapata nafasi ya kutembelea Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), hopitali kadhaa za binafsi na Kituo cha Taifa cha Uwekezaji (TIC).
Alisema uongozi wa shirika hilo tayari ulishafanya mazungumzo ya awali na uongozi wa Kampuni ya Yono Auction Mart nchini India hivi karibuni ili kushirikiana katika uwekezaji wa hospitali za kisasa hapa nchini na ujio wa viongozi hao ni hatua za kuanza kwa mchakato huo.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment