Ofisa Mtendaji Mkuu wa Tanzania Pharmaceutical Industry Ltd, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhan Madabida (kuhsoto), akiwa na wenzake
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhani Madabida, na wenzake watano wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, wakikabiliwa na mashitaka matano ya usambazaji wa dawa bandia za Kupunguza Makali ya Virusi vya Ukimwi (ARV).
Pia, wanakabiliwa na shitaka la kuisababishia Bohari Kuu ya Dawa (MSD) hasara ya zaidi ya Sh. milioni 148.3.
Madabida pia ni Mkurugenzi Mkuu wa kiwanda cha kutengeza dawa cha Tanzania Pharmaceutical Industries Limited (TPIL).
Wengine walioshitakiwa naye ni Meneja Uendeshaji, Seif Shamte, aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mpira wa Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam, ambaye pia ni Meneja Masoko, Simon Msoffe.
Wengine ni Mhasibu Msaidizi wa MSD, Fatma Shango; aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Udhibiti Ubora wa Dawa wa MSD, Sadiki Materu, na Evans Mwemezi.
Wote walisomewa mashitaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi, Nyigulila Mwaseba, ambaye amepangiwa kusikiliza kesi hiyo.
Kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 5 ya mwaka 2014, ilifikishwa jana katika mahakama hiyo saa 3:13 asubuhi, huku washitakiwa wote wakiwa chini ya ulinzi wa askari kanzu wa Jeshi la Polisi.
Walihifadhiwa kwenye chumba cha mahabusu ya mahakama kabla ya kupandishwa kizimbani.
Ilipofika saa 6:24 mchana, upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Faraja Nchimbi, akisaidiwa na Wakili wa Serikali, Shadrack Kimaro, uliwasomea mashitaka hayo.
Kimaro alidai shitaka la kwanza linamkabili Madabida, Shamte, Msoffe na Shango, ambao wanadaiwa kwamba, Aprili 5, mwaka 2011, jijini Dar es Salaam, waliuza na kuisambazia Idara ya MSD makopo 7,776 ya dawa bandia aina ya Antiretroviral.
Alidai dawa hizo zinajumuisha gramu 30 za ‘Stavudine’, gramu 200 za ‘Verirapine’ na ‘Batch’ namba OC 01.85 zikionyesha zimezalishwa Machi, 2011 na kuisha muda wake Februari, 2013.
Kimaro alidai washitakiwa hao walifanya hivyo ili kuonyesha kuwa dawa hizo ni halisi aina ya ‘Antiretroviral’ wakati wakijua siyo kweli.
Alidai shitaka la pili, ambalo linahusu usambazaji wa dawa hizo, linawakabili washitakiwa hao.
Kimaro alidai kuwa wote wanne wanadaiwa kuwa wakiwa na nyadhifa zao hizo, waliisambazia MSD makopo 4,476 ya dawa aina ya ‘Antiretroviral’.
Alidai dawa hizo zinajumuisha gramu 30 za ‘Stavudide’, gramu 200 za ‘Nevirapine’ na gramu 150 za ‘Lamivudine’ zenye ‘Batch’ namba OC 01.85 zikionyesha zimezalishwa Machi, 2011 na kuisha muda wake Februari, 2013.
Kimaro alidai kuwa washitakiwa hao walifanya hivyo kwa lengo la kuonyesha kuwa dawa hizo ni halisi aina ya ‘Antiretroviral’ wakati wakijua siyo kweli.
Alidai katika shitaka la tatu washitakiwa hao wanadaiwa kuwa kati ya Aprili 12-29, mwaka 2011, jijini Dar es Salaam, wakiwa na nia ya kudanganya, kwa pamoja walijipatia Sh.148,350,156.48 kutoka kitengo cha MSD.
Kimaro alidai kuwa washitakiwa hao walijipatia fedha hizo kutoka kitengo hicho baada ya kudanganya kwamba, fedha hizo ni malipo ya dawa halisi aina ya ‘Antiretroviral’ wakati wakijua siyo kweli.
Alidai shitaka la nne linamkabili Sadick na Evans.
Kimaro alidai washitakiwa hao wanadaiwa kuwa katika tarehe tofauti kati ya Aprili 5 na 13, mwaka 2011, jijini Dar es Salaam, wakiwa kama waajiriwa wa Idara ya MSD kama Meneja Udhiditi Ubora na Ofisa Udhibiti Ubora, huku wakijua nia ya kutendeka kwa kosa, ambalo ni kusambaza dawa bandia, walishindwa kutumia nyadhifa zao kudhibiti kosa hilo lisitendeke.
Alidai shitaka la tano linawakabili washitakiwa wote, ambao wanadaiwa kwamba, kati ya Aprili 5 hadi 30, mwaka 2011, kwa nafasi zao na kutotekeleza majukumu yao ipasavyo, waliisababishia MSD kusambaziwa dawa bandia na hivyo bohari kupata hasara ya Sh. 148,350,156.48.
Baada ya kusomewa mashitaka hayo, washtakiwa wote walikana na upande wa Jamhuri ulidai kwamba, upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.
Pia upande wa Jamhuri ulidai kwamba, hauna pingamizi na dhamana kwa washtakiwa wote.
Hakimu Mwaseba alisema washtakiwa watakuwa nje kwa dhamana kama watakuwa na wadhamini wawili wa kuaminika watakaotoa fedha taslimu Sh.12,365,513 au hati ya mali isiyohamishika yenye thamani hiyo ya fedha kwa kila mshitakiwa.
Hata hivyo, washtakiwa wawili; wa kwanza na wa tano, ambao ni Madabida na Materu walitimiza masharti hayo na kuachiwa kwa dhamana.
Lakini wengine walipelekwa mahabusu hadi Februari 24, mwaka huu, kesi yao itakapotajwa.
KASHFA YA ARV 'FEKI' ILIPOANZIA
Kashfa kuhusu ARV bandia, iliibuliwa na vyombo vya habari Septemba, mwaka jana, baada ya toleo mojawapo la dawa hizo la Machi, 2011 kubainika kuwa ni bandia.
Kiwango kikubwa cha dawa hizo, ambazo hutolewa bure na serikali katika hospitali zake ziliripotiwa kusambazwa na maelfu ya wagonjwa walishazitumia kwa kiasi kikubwa.
ARV hizo ‘feki’ zinazodaiwa kutoka nchini India, ziliingizwa kwenye mfumo, Mei, mwaka jana.
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii (kwa wakati huo akiwa naibu), Dk. Seif Seleman Rashid, alikaririwa na vyombo vya habari akisema serikali ndiyo iliyogundua kuingizwa kwa ARV hizo ‘feki’ nchini.
Taarifa nyingine zilimkariri mmiliki wa TPIL kinachotengeneza ARV, Zarina Madabida, akisema kiwanda chake ndicho kilichogundua kuwapo kwa dawa hizo.
Zarina, ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalum (CCM) alisema baada ya kugundua ARV hizo ‘feki’, alitoa taarifa kwa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) na kuiomba iingilie kati ili kuziondoa kwenye mzunguko.
Kashfa ya kusambazwa ARV bandia, ilisababisha Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Joseph Mgaya, na vigogo wengine wa MSD, kusimamishwa kazi.
Wengine waliosimamishwa kazi ni Mkuu wa Kitengo cha Udhibiti Ubora, Daud Maselo na Materu.
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii wa wakati huo, Dk. Hussein Mwinyi, alikaririwa akisema viongozi hao walisimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi kufuatia kuruhusu kusambazwa kwa ARV bandia aina ya TT-VIR 30 toleo Na.0C.01.85.
Kwa mujibu wa Waziri Mwinyi ambaye kwa sasa ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), dawa hizo zilisambazwa katika vituo mbalimbali vya kutolea huduma za afya nchini.
Mbali na viongozi na watendaji hao kusimamishwa kazi, serikali kupitia wizara hiyo pia ilisitisha kiwanda cha TPIL kuzalisha dawa hizo.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment