Vigogo wa TBA, Makumba Kimweri (kulia) na Richard Maliyaga (kushoto) wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu,Dar es Salaam (Picha na Maktaba)
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam imewahukumu vigogo wawili kulipa faini ya Sh. milioni 15 au kwenda jela miaka 15 baada ya kupatikana na hatia ya makosa matano ya ujenzi wa jengo la ghorofa 18 lililojengwa jirani na Ikulu lililopo mtaa wa Chimala Kitalu cha 45 na 46, kinyume cha sheria.
Washtakiwa hao ni aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Makumba Kimweri na aliyekuwa Msanifu Mkuu wake Richard Maliyaga (55) wote wakazi wa jijini Dar es Salaam.
Hakimu Mkazi, Sundi Fimbo, alisema baada ya kupitia ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka dhidi ya washtakiwa, mahakama imeona wana hatia kwa makosa yote matano.
Alisema hati ya mashitaka inaonyesha mshtakiwa wa kwanza anakabiliwa na mashitaka matatu na upande wa mashitaka umethibitisha kweli alitenda makosa hayo na mahakama inamhukumu kulipa faini ya Sh. milioni tatu kwa kila kosa.
Kwa upande wa mshtakiwa wa pili, hakimu alisema hakuna ubishi bila kuacha shaka mshtakiwa alitenda makosa hayo na kwamba atalipa faini ya Sh. milioni tatu kila kosa.
Alisema adhabu ya kwenda jela itakwenda sambamba na ambayo washtakiwa wataitumikia miaka mitatu.
Hata hivyo, washtakiwa walilipa faini ya Sh. milioni 15 na kuachiwa huru.
Katika kesi ya msingi, washtakiwa walikuwa wakikabiliwa na mashitaka matano ya matumizi mabaya ya ofisi katika utoaji kibali cha ujenzi wa jengo la ghorofa 15 kiwanja namba 45 mtaa wa Chimara.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment