Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas
Askari Polisi namba F.5264 PC Sabato (37), amefariki dunia baada ya kujeruhiwa kwa jiwe kichwani na mtuhumiwa wa kesi ya uvunjaji wa nyumba, Njoke Ole Kiripi (34), mkazi wa Olebomba, wilaya ya Longido, mkoani Arusha.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Tukio hilo lilitokea Februari 4, mwaka huu, saa 5:00 usiku.
Kwa mujibu wa Kamanda Sabas, mtuhumiwa huyo alikuwa akikabiliwa na kesi ya uvunjaji na alikuwa katika Mahakama ya Wilaya ya Longido.
Alisema mahakama iliamuru mtuhumiwa huyo apelekwe mahabusu Kisongo, mjini Arusha, majira ya mchana.
“Sasa kwa kuwa gari la Magereza lilikuwa limeshaondoka kurudi mjini, askari huyu alilazimika kupanda daladala na mtuhumiwa huyo kufungwa pingu,” alisema Kamanda Sabas.
Alisema walipofika eneo la Uwanja wa Ndege, mita chache kufika Gereza Kuu la Kisongo ambako alitakiwa kwenda kupumzika, alimwomba askari huyo kushuka chini ili ajisaidie haja ndogo.
“Askari huyu alimsikiliza. Na alipofika chini aliomba afunguliwe pingu na askari akamfungua pingu mkono mmoja ili aweze kujisaidia vizuri. Mtuhumiwa huyu akainama na ghafla akainua jiwe kubwa na kumpiga nalo polisi,” alisema Kamanda Sabas.
Alisema baada ya kupigwa jiwe, askari huyo alipoteza fahamu na kwa kuwa kulikuwa na waendesha pikipiki jirani na eneo hilo walimkimbiza mtuhumiwa huyo.
Kamanda Sabas alisema waendesha pikipiki hao walimkamata mtuhumiwa ambaye anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za mauaji.
Alisema askari huyo alipelekwa Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru na kwamba ilipofika saa 5:00 juzi asubuhi alifariki dunia.
Askari huyo ameacha mke mmoja na mtoto mmoja.
Kamanda Sabas alisema utaratibu wa kusafirisha mwili wa marehemu kwenda kijijini kwao Kisiwa cha Ukerewe, mkoani Mwanza kwa mazishi unafanyika.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo ambaye ni mwendesha ‘bodaboda’, Juma Abadallah, alisema alikuwa jirani na daladala iliposimama na aliona watu wawili wakishuka.
“Nilikuwa nawaangalia. Na waliposhuka, askari akamfungua pingu mkono mmoja. Na huyu kijana akainama kama anataka kujisaidia. Ila ghafla nikaona anarusha jiwe kubwa kwa askari, ambaye naye alianguka chini akiwa hana fahamu. Tukatoa taarifa polisi,” alisema.
Alisema mtuhumiwa huyo alijaribu kukimbia lakini akakimbizwa na vijana waliokuwa eneo hilo na kumkamata.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment